April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge Wanawake watoa kipigo kwa Wanahabari Wanawake goli 31-10

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Dodoma

Timu ya mpira wa pete (Netball) ya Wabunge Wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeichapa vikali timu ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa magoli 31-10 katika mchezo wa kirafiki.

Mchezo huo wa kirafiki uliunguruma katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambao waandishi wa habari walishindwa kufurukuta mbele ya wapinzani wao baada ya kukubali kichapo hicho.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson ameipongeza timu ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa uthubutu wa kuweza kucheza licha ya kuonekana kutokuwa na mazoezi.

Dkt.Tulia amelezea siri ya ushindi wao katika mchezo huo ni ufanyaji wa mazoezi huku akiwapongeza waandishi wa habari wanawake Tanzania kwenda kushirikiana nao katika kucheza mchezo huo.

“Nitoe Siri mtu alitaka kutufunga aje kipindi cha mwanzo mwanzo kidogo cha Bunge,sasa hivi hapa tumeisha Kaa zaidi ya mwezi tumeisha fanya mazoezi,tumefurahi sana waandishi wa habari Wanawake Tanzania kuja kushirikiana nasi kufanya mazoezi, mazoezi ni afya,furaha, upendo tumewafunga lakini tunaamini mtaendelea kujifunza na kufanya mazoezi zaidi na siku nyingine mkicheza na wabunge mjipange,”amesema Dkt Tulia.

Pia amesema Chama cha Netball Tanzania kimepata uongozi mpya,anaamini kitakuja na mkakati mzuri wa kuendeleza mchezo huo ili uende vizuri kama ilivyo kwa mchezo wa mpira wa miguu hivyo wale wanaopenda kucheza waanze wakiwa wadogo na waendelee kuweka bidii huku kwa upande wao wataendelea kutoa ushirikiano.

Kwa upande wao wachezaji wa timu ya mpira wa pete ya Waandishi wa Habari Wanawake akiwemo Janeth Matondo,ameeleza kuwa mchezo ulikuwa mzuri ingawa ulikuwa mgumu.

“Mchezo ulikuwa mgumu siyo kwa sababu nilikuwa namkaba Spika,lakini sisi waandishi wa habari tunatoka mikoa mbalimbali nchini hivyo hatuna mazoezi ya pamoja ya muda mrefu,hatukupa fursa ya mazoezi ya kusema tukae kambini hata wiki moja kiukweli leo wangelia wametufunga lakini kwa tabuu sana,”ameeleza Matondo.

Hata hivyo waandishi wa habari Wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini wamefanya ziara ya siku mbili jijini Dodoma ambapo walipata fursa ya kuhudhuria Bunge na kujifunza namna shughuli za Bunge zinavyofanyika pamoja na kucheza mchezo huo wa kirafiki wa mpira wa pete.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson,akizuia mchezaji akitupia mpira katika goli la wapinzani wao,katika mchezo wa kirafiki wa mpira wa pete uliotuma vumbi katika uwanja wa Jamhuri kati ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania na Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na Judith Ferdinand)
Mchezaji wa timu ya mpira wa pete ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Janeth Matondo ( aliyeshika mpira) akikimbia huku Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson,akijaribu kumkabili mchezo wa kirafiki wa mpira wa pete uliotimua vumbi katika uwanja wa Jamhuri kati ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania na Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na Judith Ferdinand)
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Ackson,akizuia mchezaji akitupia mpira katika goli la wapinzani wao,katika mchezo wa kirafiki wa mpira wa pete uliotimua vumbi katika uwanja wa Jamhuri kati ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania na Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na Judith Ferdinand)
Wachezaji wa timu ya mpira wa pete ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania pamoja na timu ya Wabunge Wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwemo Spika wa Bunge Dkt.Tulia Ackson wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo wa kirafiki uliofanyika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.(,Picha na Judith Ferdinand)