June 1, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Magu bingwa UMITASHUMTA

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza imeibuka bingwa wa jumla wa mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya mkoa yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Nsumba.

Katika mashindano hayo, Wilaya ya Nyamagana ilishika nafasi ya pili, ikifuatiwa na Misungwi iliyomaliza nafasi ya tatu, huku Buchosa ikishika nafasi ya nne.

Sengerema ilimaliza nafasi ya tano, Ilemela nafasi ya sita, Ukerewe nafasi ya saba na Kwimba ikamaliza katika nafasi ya nane.

Akizungumzia maandalizi ya mashindano ya taifa, Ofisa Michezo wa Mkoa, James William, amesema mkoa wa Mwanza umejipanga vyema kuhakikisha unapata ubingwa wa tano mfululizo katika mashindano yatakayofanyika kuanzia Juni 5 hadi Juni 17 katika Chuo cha Ualimu Kleruu, Iringa.

Amesema maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha na timu ipo tayari kuwakilisha mkoa huo kwa ushindani mkubwa dhidi ya mikoa mingine nchini.

William amesema Mwanza itapeleka jumla ya wachezaji 120 pamoja na walimu 19 watakaosimamia na kufundisha timu katika michezo mbalimbali.

Ameongeza kuwa timu hiyo inaongozwa na Mratibu Mkuu Joseph Mambo, huku Amina Msabila akiwa matron na Masumbuko Sagiza akihusika katika usimamizi wa timu.

William amesisitiza kuwa lengo kuu ni kutetea ubingwa na kuendelea kuandika historia ya ushindi mfululizo, akisema wachezaji wote wameonyesha kiwango kizuri na nidhamu ya hali ya juu.