Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza.
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wanafunzi kushiriki kikamilifu katika michezo bila kuacha kuzingatia masomo, akisisitiza umuhimu wa kujenga kizazi chenye maarifa, nidhamu na afya bora.
Mtanda amesema hayo, wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA uliofanyika katika shule ya sekondari Nsumba mkoani Mwanza.

Amesema pamoja na ushindani uliopo katika mashindano hayo, wanafunzi wanapaswa kuelewa kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha yao ya baadaye na mafanikio yao.
“Michezo na elimu lazima viende sanjari hivyo tunahitaji vijana wanaofanya vizuri darasani na pia katika michezo,” amesema Mtanda.
Aidha, amewataka vijana kutumia fursa za michezo kujijengea maisha bora na kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya elimu, ubunifu na kuongeza maarifa.
Pia amewahimiza walimu na makocha kuhakikisha wanawaandaa vizuri wanafunzi ili Mkoa wa Mwanza ufanye vizuri katika mashindano ya kitaifa yatakayofanyika Chuo cha Ualimu Klerruu mkoani Iringa.
Mashindano ya UMITASHUMTA yataanza Juni 5 hadi 17 mwaka huu, huku UMISSETA yakitarajiwa kufanyika kuanzia Juni 18 hadi 30.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, James William, amesema mkoa huo utawakilishwa na wachezaji 120 watakaounda timu ya mkoa katika mashindano hayo.
Amesema michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na soka kwa viziwi, mpira wa kengele, riadha maalum, netiboli, mpira wa mikono na mpira wa wavu, ikilenga kutoa nafasi sawa kwa wanafunzi wote.
William amesema Mwanza imeendelea kufanya vizuri katika UMISSETA kwa kutwaa ubingwa kwa miaka miwili mfululizo na kuwataka wadau kuendelea kusaidia kuboresha miundombinu na vifaa vya michezo ili kukuza vipaji vya vijana zaidi.


More Stories
CHADEMA yakaribishwa kujifunza siasa kwa Kihongosi
Wizara yasikitishwa na upotoshaji wa Bajeti 2026/27
Tuzo za Waandishi wa Habari za Hali ya Hewa zazinduliwa