June 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara yasikitishwa na upotoshaji wa Bajeti 2026/27

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema imesikitishwa na vitendo vya upotoshaji wa taarifa pamoja na usambazaji wa matamshi yasiyo sahihi yanayoendelea kusambazwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii kufuatia Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Hotuba hiyo iliwasilishwa Bungeni jijini Dodoma Mei 26, 2026 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa leo jijini Dodoma, Wizara hiyo imeleza kuwa baadhi ya taarifa zinazosambazwa mitandaoni zimepotosha kwa makusudi maudhui halisi ya hotuba hiyo kwa lengo la kuleta mkanganyiko kwa umma pamoja na kuathiri taswira ya Tanzania na misingi ya diplomasia, uhuru na mshikamano wa kitaifa.

Wizara imeeleza kuwa kutokana na hali hiyo itaendelea kutoa ufafanuzi rasmi kupitia vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zenye kueleza kwa usahihi msimamo wa Serikali kuhusu masuala yaliyojadiliwa katika hotuba hiyo.

Aidha, Wizara imeipongeza vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa kuendesha mjadala mpana wa kitaifa kuhusu hotuba hiyo, jambo lililodhihirisha mshikamano wa kitaifa pamoja na kuonesha uungwaji mkono wa kauli zilizotolewa na wabunge mbalimbali wakati wa kuchangia hotuba hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mijadala hiyo imeonesha umuhimu wa kulinda uhuru, hadhi na utaifa wa Tanzania, hasa katika kipindi ambacho kumekuwa na mijadala ya kimataifa kuhusu misimamo ya baadhi ya mataifa ya nje kuhusiana na masuala ya ndani ya nchi nyingine.

“Wizara inatambua kuwa kuwepo kwa mjadala huo ni ishara ya ukomavu wa diplomasia yetu, demokrasia na uzalendo wa Watanzania katika kusimamia maslahi ya Taifa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia kwa uthabiti misingi ya uhuru wa Taifa, heshima ya nchi, kutokuingiliwa katika mambo ya ndani pamoja na kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia unaozingatia usawa, heshima na maslahi ya pande zote kwa mujibu wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

Sambamba na hilo, Wizara imetoa wito kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, wadau wa habari na wananchi kwa ujumla kutumia uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia weledi, maadili, sheria za nchi pamoja na kulinda mshikamano na heshima ya Taifa.