
Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Kilimanjaro
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaalika vyama vya upinzani kesho, Mei 29, 2026 kujitokeza katika mikutano yake kusikiliza na kujifunza jinsi ya kufanya siasa za kistaarabu kutoka kwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Patrick Boisafi, amesema, CCM ni chama pekee kilichojikita katika kufanya siasa za kistaarabu ikiwa pamoja na kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi pamoja na kuwatatulia changamoto zao.

Akizungumza na waandishi hao, Boisafi ametoa wito kwa vyama hivyo vya upinzani kikiwemo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kutumia mikutano hiyo ya Mwenezi wa CCM, Kihongosi, kujifunza kufanya siasa za hoja pamoja na utatuzi wa kero ambazo zimekuwa zikiwasilishwa na wananchi katika mikutano yake, huku zingine akizitatua papo hapo.
“Natoa wito kwa wananchi wote wa kilimanjaro na vyama vyote vya upinzani, tunawakaribisha waje wenyewe wajionee jinsi mwenezi wetu wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi jinsi anavyofanya siasa za hoja tofauti na wao ambao wamekuwa wakifanya siasa za matusi”, amesema Boisafi.
Pia amesema kuwa, hivi sasa CCM katika mkoa huo, imekuwa ikifanya vizuri tofauti na awali, ambapo mkoa huo ulikuwa ukishindwa katika chaguzi mkuu na kushinda vyama pinzani.
” kwa sasa hivi tangu 2020 CCM katika mkoa huu wa Kilimanjaro imekuwa ikifanya vizuri tofauti na awali kwani tulikuwa waathirika..sasa hivi kwanza mtu unaweza kwenda hata kanisani na sare yako ya CCM na baadae ukaingia nayo kwenye mkutano wa chama”, amesema Boisafi.
Ikiwa ni muendelezo wa ziara za Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi, nchini, akiwa amemaliza katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na leo kunza katika Mikoa ya Kaskazini.
Leo anaanza ziara yake mkoani Kilimanjaro, akianza na Wilaya ya Siha, ambapo atapokelewa na wachama wa CCM katika wilaya hiyo na kutembelea Shina namba tisa kisha atatembelea Shule ya wasichana ya Kilimanjaro, Hospitali ya Kibong’oto na mwisho atafanya mkutano wa hadhara katika eneo la Sanya Juu, ambapo atasikiliza na kutatua kero za wananchi.

More Stories
Mtanda ahimiza uwiano kwenye michezo,masomo.
Wizara yasikitishwa na upotoshaji wa Bajeti 2026/27
Tuzo za Waandishi wa Habari za Hali ya Hewa zazinduliwa