April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vifaranga vya kuku

Vifaranga vya kuku vyaadimika Kisutu

Na Mwandishi Wetu

WAFUNGAJI wameshtushwa na ongezeko la bei ya vifaranga vya kuku kutoka sh. 1,200 kwa kifaranga kimoja hadi sh. 2,000, hali inayoashiria uwezekano wa kupanda kwa bei ya kitoweo hicho.

Baadhi ya wananchi waliozungumza jana wamesema kutokana na uhaba huo, wanalazimika kununua vifaranga kwa bei ya juu.

Muuza kuku, Ramadhani Ally kutoka soko la Kisutu jijin Dar es Salaam alisema biashara hiyo kwa sasa sio nzuri kulingana na idadi ya kuku waliopo sokoni.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo uhaba huo wa vifaranga unatajwa kusababishwa na janga la Corona. “Janga la Corona limechangia kuadimika bidhaa ya kuku sokoni,” alisema na kutoa wito kwa wazalishaji wa kuku ikiwemo Interchick kuongeza uzalishaji zaidi ili kwenda sambamba na mahitaji ya sokoni kwa sasa.

“Wiki mbili kabla ya sasa kwa siku za mwanzoni tulikuwa tunauza kuku 150 hadi 100 kwa siku, lakini mauzo hayo sasa yamebaki kama historia, kwani mauzo yameshuka hadi kufikia kuku 50 kwa siku,” alisema na kuongeza kuwa kuku mmoja sh. 6,500.

Alisema wanunuzi wa kuku wanategemea sana hali ya soko la wauuzaji na idadi mauzo huongezeka kulingana na mahitaji ya siku hiyo, kwani kama soko ni zuri muuzaji anaweza kununua kuku 500 kwa siku na akawauza wote.

Kwa mujibu wa wa mfanyabiashara huyo wateja wa kuku wamepungua ikilinganishwa na siku za nyuma.

“Wateja wanakuja mara moja, lakini hawarudi tena baada ya ushuru kupanda kutoka sh. 500 hadi sh.1, 000 kwa siku, hivyo kila mfanyabiashara anayemiliki banda anatakiwa kulipa ushuru sh. 30,000 kila mwezi bila kujali umeuza au hujauza kuku kwa mwezi huo,” alisema Anuary Yusuph.

Alitoa angalizo kwa baadhi ya vijana ambao wapo kwenye biashara hiyo kuwa wavumilivu, kwani huenda hali hii ikabadilika na changamoto hiyo ikatoweka kabisa.

Naye Mtunza Hazina wa Soko la Kisutu, Ally Vulu ,alisema idadi ya wauza kuku ambao wanalipa ushuru wa sh. 1,000 ni zaidi 120, hivyo alishauri ushuru huo upunguzwe kwani hali ya biashara kwa sasa ni mbaya.

Aliongeza kuwa upungufu kwa wateja na wanunuzi wa kuku ambao kwa kiwango kikubwa ni akina mama lishe, wauza chips na watu mbalmbali.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Soko la Kisutu, Zuberi Luono amedhibitisha kuwepo kwa hali hiyo sokoni hapo na kuziomba mamlaka serikalini hususani Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha uzalishaji wa vifaranga nchini unaongezeka.