May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usalama pambano la Dulla Mbabe, Twaha Kiduku mikononi mwa mwamuzi, majaji

Na Halfan Diyu, TimesMajira Online

USIKU wa deni haukawii kukucha ni msemo maarufu ambao hutumika na watu wa rika mbalimbali wakijaribu kuelezea namna saa zinavyokimbia kwa kasi, wakati kuna jambo zito au linalomtatanisha au kumkabili mtu husika.

Leo Agosti 28 ni tarehe ambayo imekuwa ikiimbwa na vyombo mbalimbali vya habari, yakiwemo magazeti, runinga, redio, blogu na maendeo mbalimbali wakielezea kuhusu pambano kati ya mabondia wanaofanya vizuri hapa nchini Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Twaha Kassim ‘Kiduku’.

Mabondia hawa wanaofanya vizuri hapa nchini wamekuwa wakitambiana kwa muda mrefu huku pambano lao la leo usiku likiwa ni moja ya mapambano ambayo yametangazwa sana na kupambwa na kila aina.

Ubishi huo unakwenda kumalizwa leo katika pambano lao la kuwania ubingwa wa Taifa la raundi 12 uzito wa Super Middle litakalochezwa katika uwanja wa Uhuru.

Awali ubishi huo ulishindwa kumalizwa Oktoba 21 mwaka 2017 katika ukumbi wa Msasani ‘Msasani Club’ baada ya pambano lililowakutanisha wawili hao kumalizika kwa sare ya pointi.

Ni vema pambano hili likasimamiwa kikamilifu kwa kufuata sheria zote za mchezo wa ngumi sambamba na kuzingatia ulinzi wa kutosha ,ili kumpata mshindi ambaye hatalalamikiwa.

Majaji wana nafasi tena ya kuudhihirishia umma wa mchezo wa ngumi kuwa si wa ubabaishaji kwa kutenda haki kwa kutoa alama sahihi kwa kila raundi na si kuongozwa na hisia za kishabiki au itikadi yoyote ile hali inayoweza kusababisha vurugu.

Maamuzi mabaya ya majaji yanaweza kusababisha vurugu katika pambano hilo ambalo watanzania wengi wanalifuatilia kwa karibu kuona nani kweli ni mwamba wa mwenzake baada ya kutambiana kwa muda mrefu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Pia mashabiki wa ngumi wanataka kuona bondia atakayecheza vizuri aidha kwa kupata pointi nyingi kwa raundi zote au kushinda kwa Technical Knock out ndiye anatangazwa mshindi.

Kutenda haki kwa majaji wa pambano hilo kutaongeza heshima kubwa katika mchezo wa ngumi na hata kuwafanya sasa wadhamini kujitokeza kwa wingi kudhamini mchezo huo ambao unaopendwa na watanzania wengi baada ya mchezo wa soka.

Pia waandaaji wahakikishe usalama unakuwepo wakati wote, kabla mabondia kupanda ulingoni, wakati wa mchezo wenyewe, muda wa kutangaza matokeo na baada ya mchezo kumalizika ili kuwafanya walioenda uwanjani kutazama pambano hilo wanarudi makwao kwa usalama kabisa.

Katika siku za nyuma tumeshashuhudia mapambano ya namna hii yaliyojaa ushabiki na hisia kali kwa mashabiki wa mabondia na hatimaye vurugu hutokea na pambano kushindwa kuendelea mfano wa pambano la Francis Cheka dhidi ya Japhet Kaseba kwenye uwanja huo huo wa Uhuru.

Leo Kiduku na Dullah Mbabe wameshawagawa mashabiki wa mchezo huo, hakuna shabiki anayekubali kuwa bondia wake atapoteza pambano hilo na kila mmoja anaamini bondia wake yupo vizuri kushinda pambano hilo huku wakisahau kabisa kuwa katika mchezo wowote ule kushinda au kushindwa ni sehemu ya mchezo.

Kwa mabondia hawa, nawashauri wacheze ngumi kwa weledi, wasicheze kama wanagombana bali wafuate sheria za mchezo huo, waachane na rafu za makusudi katika mchezo wao jambo ambalo linaweza kusababisha mchezo huo kuvunjika au kutokuwa wa kuvutia kwa mashabiki watakaokuwa wakitazama pambano lao lazima waoneshe mashabiki kuwa wao ni mabondia mahiri.

Lazima wakubaliane na matokeo ya haki yatakayotolewa na majaji, hakuna haja ya kuanza kuleta vurugu mara baada ya kuona mmoja wao amepoteza kwa kuhujumiwa bali wazingatie usalama wao na wa mashabiki wa ngumi ili kuupa heshima mchezo huo.

Binafsi naamini mabondia wote ni wakali na wana uwezo mkubwa katika kurusha masumbwi na kuhimili masumbwi hivyo usalama na amani ya pambano lao upo chini yao, hilo walizingatiwe sana, wasiongozwe na hisia na makelele ya mashabiki wao kuharibu pambano hilo.

Kwa mashabiki wa mchezo wa ngumi, baadhi yao wamekuwa ni watu wenye kupenda vurugu huku wakishindwa kujua kiutaalamu kwanini bondia wao kapoteza pambano husika, wamekuwa wakitoa maneno makali dhidi ya mwamuzi au majaji lakini tu niwashauri kuwa wanapaswa kubadilika kwa kuutendea heshima mchezo huo.

Watambue hakuna bondia yeyote Dunia asiyepigwa, walipigwa kina Mohamed Ali, Rashid Matumla, Francis Cheka, Lennox Lewis, Evander na wengineo ambao walitamba vilivyo katika ulingo wa ngumi, hivyo waondokane na dhana kuwa bondia wao ni mtu wa kushinda tu.