May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Maji Bonde la Kati yaamzisha jumuiya za watumiaji maji

Na Dotto Mwaibale,TimesMajira,Online Shinyanga.

BODI ya Maji Bonde la Kati kwa kushiriana na viongozi wa vijiji na kata ambao ni wawakilishi wa wananchi wanaotumia Bwawa la Nhumbu wamefanikiwa kuanzisha jumuiya ya watumia maji kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji mkoani Shinyanga.

Akizungumza juzi kuhusu huanzishwaji wa jumuiya hiyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa Bodi ya Maji Bonde la Kati, Nelea Bundala, amesema jumuiya hiyo itasaidia kulinda vyanzo vya maji ambavyo vinaharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo zinazofanyika mpaka ndani ya bwawa hilo.

Amesema kwa kuwa wao kazi yao kubwa ni kusimamia rasilimali za maji ili ziwe endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo wameona ni muhimu kuwepo na jumuiya ya watumia maji hususani kwa kuanzia Bwawa la Nhumbu na baadae Bwawa la Songwa na mengine ili kuhakikisha yanadumu na wanayatumia kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Bundala amesema sheria inaelekeza kwamba mtumiaji wa maji ndiye mtunzaji namba moja wa maji kwa sababu ni mnufaika na yupo maeneo ya vyanzo vya maji husika.

Amesema wametembea kwenye vijiji hivyo na kufanya mikutano na kupata wawakilishi watatu kutoka katika kila kijiji wakiwakilisha kundi la wafugaji, wakulima na watumiaji wa maji na kuwa sasa wanamalizia mchakato kwa kukamilisha kuunda jumuiya hiyo baada ya kutoa mafunzo ya siku tatu ili waweze kujua sheria na sera ya maji inasemaje na majukumu yao ya kusimamia rasilimali ya maji.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa Bodi ya Maji Bonde la Kati, Hhau Swarwatt, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Buchambi juzi katika mkutano wa hadhara wa mchakato wa kupata wawakilishi watatu ambao wataunda Jumuiya ya Watumia Maji wa Bwawa la Nhumbu ambayo itakuwa ikifanya kazi ya kulinda vyanzo vya maji mkoani Shinyanga. Picha na Dotto Mwaibale.

Amesema mchakato huo uwe wamewashirikisha viongozi wa vijiji kwa sababu wao ni walinzi wa amani, wasimamizi wa kuu ngazi za vijiji hivyo jumuiya haiwezi kufanya kazi peke yake bila ya kushirikiana na vijiji.

“Viongozi wa vijiji na wawakilishi wa vijiji kwa pamoja tumekaa darasani tukiamini tutakuwa na uelewa wa pamoja tukianzia kwa viongozi na wana jumuiya wenyewe wanaozunguka mabwawa hayo,” amesema Bundala.

Bundala amesema katika mchakato huo wamewashirikisha wadau wengine kama Williamson Diamonds Limited wanao miliki Mgodi wa Almasi wa Mwadui na Bwawa la Nhumbu, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Manispaa ya Shinyanga, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Meneja wa Maji Safi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kishapu lengo likiwa kuunda jumuiya hiyo ambayo itakuwa ikisimamia rasilimali za maji katika maeneo hayo.

Amesema baada ya hapo wajumbe watakuwa na katiba na mpango kazi na rasimu ya katiba ambayo watarudi nayo vijijini na kuipitisha kwa wananchi ili waielewe kabla haijawa katiba rasmi na hatimaye wataizindua jumuiya hiyo ili iweze kufanya kazi yake.

Amesema lengo ni kuhakikisha kama wizara ya maji wadau wanaielewa sera, sheria na kuunda vyama vya watumia maji viweze kuhakisha vinafanya kazi kwa niaba ya bonde kusaidia wizara kutunza mazingira na vyanzo vya maji.