April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubalozi wa Marekani waandaa Kongamano kwa wajasiriamali 150

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. dar

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni,Saad Mtambule, leo Aprili 15, 2024 Jijini Dar es Salaam, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwenye Kongamano lililohusisha wajasiriamali wanawake 150 kutoka mikoa 9 ya Tanzania bara na Unguja.

amesema, Mkoa wa Dar es Salaam utaendelea kutoa ushirikiano kwa wajasiriamali wote, hususani wanawake wanaofanya shughuli zao katika mkoa wa Dar es Salaam, ili waweze kujipatia kipato kitakacho wainua kiuchumi na kuendesha familia zao.

Katika Kongamano hilo lililoandaliwa na Ubalozi wa Marekani, lengo likiwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali hao, Mtambule amesema, moja ya mikakati ya Serikali ni pamoja na kuwainua wanawake wajasiriamali kiuchumi, ili waweze kuendesha maisha yao vizuri pamoja na kuleta chachu ya maendeleo katika Taifa.

” Lengo la Serikali kupitia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wajasiriamali hususani wanawake wanaungwa mkono katika shughuli zao za kujipatia kipato ikiwa pamoja na kuwatengenezea mazingira rafiki kwa ajili ya shughuli zao na ndiyo maana Rais Samia alianzisha na jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi, hivyo na sisi kama watumishi wake tunamuunga mkono kwa kufanya yale aliyodhamilia kwa wananchi wake kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla”, amesema Mtambule.

Aidha ameongeza kuwa, upo mpango wa Jiji la Dar es Salaam, kurasimisha ” Mama Ntilie” ili waweze kutambulika, lengo likiwa ni kupata data kamili kuhusu wao, hali itayowarahisisha kupata mikopo katika Taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Nao baadhi ya washiriki, akiwemo, Magreth Masonga, ambaye ana Mmiliki shule ya awali ya mcheluo wa kingereza, amesema elimu ya ujasiriamali aliyoipata Awe imeweza kumsaidia kutika kusimamia shule yake, ” kwa kweli Awe imenisaidia katika mambo mengi ya ujasiriamali, kwani elimu niliyoipata pale ikiwa pamoja na elimu ya kupanga bei hakika imeniimarisha kimaisha.

Hivi sasa nasimamia maisha ya gu kupitia biashara yangu, kwani nimeweza kuajili wafanyakazi ambao ni walimu, watu wa usafi nk na yote ni kwasababu ya kusimama kwa shule hiyo na endapo kama nisingekuwa na elimu ya ujasiriamali sidhani kama ningeweza kusimamia kwa faida shule hiyo”, anasema Masonga.

Nae, Shamsa Kileo, ambaye amejikita katika shughuli za kilimo amesema, kwa upande wake anaushukuru Ubalozi wa Marekani kwa kuandaa semina hiyo, ambayo anahakika itaenda kuinua wanawake wengi wajasiriamali ikiwa pamoja na kuwaongezea ujuzi katika shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato.