April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BOT yaendesha warsha kwa wadau wa sekta ya fedha

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha warsha ya pili kwa wadau wa Sekta ya Fedha kuhusu masuala ya Usalama wa Mifumo ya TEHAMA na Mitandao ya Mawasiliano kwa Timu ya Mwitikio wa Kukabili Majanga ya Kompyuta ya Sekta ya Fedha Tanzania (TZ- FinCERT).

Akifungua warsha hiyo iliyofanyika Benki Kuu jijini Dar es Salaam tarehe 16 Aprili 2024, Naibu Gavana wa BoT (Utawala na Udhibiti wa Ndani), Julian Banzi Raphael, amesema inalenga kujadili taratibu za kuripoti na kushirikiana katika masuala ya Usalama wa Mifumo ya TEHAMA na Mitandao ya Mawasiliano, ili kukabiliana vyema na matukio ya Usalama wa Mifumo ya TEHAMA na Mitandao ya Mawasiliano kama Jumuiya ya TZ- FinCERT.

Amesema kuwa matumizi makubwa ya Mifumo ya TEHAMA na mabadiliko ya kidigitali yamesababisha kuwepo kwa changamoto mpya katika Sekta ya Fedha.

“Benki Kuu kwa kutambua changamoto hizo imeona umuhimu wa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha na kuanzisha Timu ya TZ – FinCERT kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta yaani Electronic and Postal Communication Act (EPOCA) ya Mwaka 2010”, alisema.

Kuanzishwa kwa TZ-FinCERT kunaonesha juhudi za pamoja za kuimarisha sekta ya Fedha katika kugundua, kutathimini na kujibu kwa wakati matukio ya Usalama wa Mifumo ya TEHAMA na Mitandao ya Mawasiliano na hivyo kupunguza athari ambazo zinaweza kutokea katika sekta ya fedha.