May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mwakyembe awataka waandishi kudumisha Amani.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison   Mwakyembe amevitaka Vyombo vya Habari Nchini kuendelea kudumisha na kulinda amani katika kipindi chote cha kampeni mpaka Uchaguzi Mkuu  kwa kuandika na kutangazia  umma habari ambazo zina ukweli.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo jana alipokua akifanya mahojiano na vyombo vya habari vya redio na runinga vinavyomililikwa na taasisi ya “ISLAMIC FOUNDATION” ambavyo ni redio Imaan na TV Imaan pamoja kuzungumza na Wadau wa Sekta ya Habari Mkoani  Morogoro.

Waziri  Mwakyembe amesema wanahabari wana nafasi ya kulinda au kubomoa amani ya nchi kupitia kalamu zao kama wasipozitumia vizuri, huku akitolea mfano nchi ambazo ziliingia katika machafuko kupitia vyombo vya habari.

“Mwanahabari ni mwalimu, mfasili, mkalimani, mchambuzi na mtetezi hivyo ni vizuri akatumia taaluma yake vizuri katika kuhabarisha umma ili asilete migogoro, Pia mwanahabari anapaswa kuelezea sera za wagombea na vyama vyao ili kuisaidia jamii kutambua mgombea sahihi na kuchagua mgombea bora”,alisema Mhe. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa kuwa ifikapo mwaka 2021 hakuna Mwandishi wa Habari yoyote ambaye kama atakuwa hajakidhi vigezo vya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2017, ataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari, lengo likiwa ni kuifanya taaluma hiyo kutambulika na kuheshimika.

Nae  Mkuu wa Mkoa wa Mororgoro Mhe.Loata Olesanare amesema mkoa huo unafanya vizuri katika sekta zote za Wizara hiyo ikiwemo kuhifadhi na kulinda mila na desturi pamoja na kulinda maeneo yote ya kiutamaduni yalipo mkoani hapo.Ambapo Tanzania inaelekea kufanya Uchaguzi Mkuu wa Urais, Wabunge na Madiwani ifikapo tarehe 28 mwezi wa 10  mwaka 2020.