April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tulia Marathon 2026 kuanza rasmi Mbeya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Mbeya

TAASISI isiyo ya kiserikali ya Tulia Trust, inayoongozwa na Dkt. Tulia Ackson, imeanza rasmi maandalizi ya mashindano ya mbio za Tulia Marathon 2026, yatakayofanyika kwa msimu wa kumi, yakitarajiwa kushirikisha zaidi ya wanariadha 5,000 kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Machi 23, 2026, Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa taasisi hiyo, Joshua Mwakanolo, amesema Watanzania wote wanakaribishwa kushiriki katika mashindano hayo yanayojulikana kama Mbeya Tulia Marathon.

Amesema mashindano hayo yatafanyika kwa siku mbili kuanzia Mei 15 hadi 16, 2026, katika Uwanja wa Sokoine.

“Mashindano ya tarehe 15 yatakuwa ya uwanjani (track events) kuanzia mita 100 hadi 1500, huku tarehe 16 yakihusisha mbio ndefu za kilometa 5, 10, 21 na 42,” amesema Mwakanolo.

Aidha, amesema kutakuwepo na burudani mbalimbali ili kuongeza hamasa kwa washiriki na watazamaji, hatua itakayochochea shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Mbeya kutokana na ongezeko la wageni.

Kwa upande wa usajili, Mwakanolo amesema vituo mbalimbali vimeandaliwa ikiwemo Uyole, ofisi za Tulia Trust, Mwanjelwa, pamoja na mikoa ya Arusha (Uwanja wa Sheikh Amri Abeid), Tukuyu na Kyela.

Ameeleza kuwa lengo kuu la mashindano hayo ni kusaidia jamii, ambapo mapato yatokanayo na tukio hilo hurejeshwa kwa wananchi kupitia miradi ya kijamii kama ujenzi wa shule, miundombinu ya afya na huduma nyingine muhimu.

Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo, Lwiza John, amesema watoto wadogo nao watapata fursa ya kushiriki kupitia mbio za mita 50, 100, 200 na 400, ikiwa ni mkakati wa kukuza vipaji vya michezo tangu utotoni.

Naye Mratibu Mkuu wa Michezo kutoka Tulia Trust, Lugano Mwangosi, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika kukuza vipaji vya michezo kupitia programu mbalimbali ikiwemo vilabu vya jogging na mazoezi ya viungo kwa kushirikiana na vyama vya michezo vya wilaya.

“Tupo tayari kuvibaini na kuvikuza vipaji vya michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” amesema Mwango.