April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waomba huduma kituo cha polisi Mabatini irejee 

*RPC Mwanza aridhia ombi hilo, asisitiza jukumu la kuzuia uhalifu ni la wote

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Wananchi wa Kata za Mabatini na Mbugani, Wilaya ya Nyamagana, mkoani Mwanza,wameomba kurejeshwa huduma za kipolisi kituo cha Polisi Mabatini kilichoharibiwa wakati wa vurugu zilizojitokeza  Oktoba 29, 2025.

Ombi hilo wamelitoa mbele ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 22,2026,uwanja wa shule ya msingi Mabatini “B”, uliowakutanisha wananchi wa kata hizo mbili na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na wananchi kupitia mkutano huo, Mutafungwa,amesema amesikia kilio chao cha muda mrefu,hivyo  aliwahakikishia kurejesha huduma hiyo,kwa kuwa wenyewe waliamua kukikarabati kituo hicho kilichoharibiwa na kuchomwa moto.

Mutafungwa amesema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa jukumu la kuzuia uhalifu si la Jeshi la Polisi  wala  viongozi wa Serikali za Mitaa pekee yao, bali ni jukumu la wote kwa sababu wahalifu wanatoka miongoni mwa jamii.

Huku akisisitiza kuwa watawadhibiti wahalifu kwa kukataa uhalifu, na ni lazima wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza waelewe dhana hiyo.

Pia,amesema jeshi hilo litaendelea kuviunga mkono vikundi vya vijana vitakavyoanzishwa na Wakaguzi wa Kata vitakavyoshiriki katika michezo mbalimbali.Kwani Jeshi la Polisi lina utaratibu wa kuzuia uhalifu kupitia michezo (Youth and Sports).

Aidha amesema,jeshi la hilo limeamua kutoka ofisini baada ya hali ya mkoa kuwa shwari na sasa wanaenda kuwafuata wananchi waliko ili wasaidiane kuzuia na kudhibiti uhalifu.

“Tunataka siku moja wananchi wafike vituo vya polisi kusalimia tu, lakini siyo kwa ajili ya changamoto za kiusalama,”amesema Mutafungwa.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa mitaa sita ya kata hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mabatini, Paulo Mpozemenya,amesema wamefanya jitihada za kukarabati kituo hicho na wameomba Kamanda aridhie kukifungua ili huduma zirejee kama awali, kwani matukio ya uhalifu yameanza kuongezeka.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Kata hiyo, Mkaguzi (Insp.) Shaban Kashakala,amesema Kata ya Mabatini ina jumla ya vikundi sita vya ulinzi vilivyo chini ya viongozi wa mitaa husika, na kazi yake imekuwa ni kutoa elimu ya namna ya ulinzi shirikishi na ukamataji salama.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana (OCD), SSP Virginia Sodoka,amewashukuru wananchi wa Kata za Mabatini na Mbugani kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia na kudhibiti uhalifu.