May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANROADS Songwe yapewa bil. 40/-za miradi miaka mitatu ya Samia

Na Moses Ng’wat, TimesmajiraOnline,Momba

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) katika Mkoa wa Songwe, imepokea wastani wa sh. bilioni 40 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za mkoa, barabara kuu pamoja na madaraja.

Fedha hizo zimetolewa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassa.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga.

Kabla ya kuyasema hayo, wakazi wa vijiji vya kata za Chitete na Msangano katika Wilaya ya Momba, Mkoani Songwe, waliishukuru Serikali kupitia TANROADS Mkoa wa Songwe kwa kufanikiwa kumaliza changamoto ya maeneo korofi ya barabara ya Igamba – Msangano hadi Chitete yenye urefu wa kilometa 87.4.

Kwa sasa barabara hiyo inapitika kwa kipindi chote cha mwaka, ikiwemo ujenzi wa daraja la mto Nkala.

Wananchi hao kutoka katika bonde maarufu kwa kilimo cha mpunga la Msangano ambako pia kuna skimu kubwa za umwagiliaji, walisema daraja hilo lililojengwa kwa gharama ya sh. milioni 527, ambapo limerahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao yao kwenda kwenye masoko.

Wametoa shukurani hizo hizo hivi karibuni katika mahojiano Majira yaliyolenga kujua namna Serikali ya awamu ya sita ilivyofanikiwa kutatua changamoto mbalimbali ndani ya miaka mitatu ya Rais Samia.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Chilulumo, Henricko Sinkala, akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, aliipongeza Serikali ya kwa namna ilivyoweza kumaliza changamoto ya daraja hilo, ambapo zamani lilikuwa likisababisha maafa kwa watu kupoteza maisha, ikiwemo mifugo yao kusombwa na maji.

Naye, Gerald Emanuel, Mkazi wa Chitete alisema kukamilika kwa daraja hilo kwa kiasi kikubwa imesaidia wao kusafirisha mazao yao kutoka kijijini hadi kwenyhe masoko yenye bei nzuri katika miji ya Mlowo na Tunduma.

Akifafanua hilo, Mhandisi Bishanga, amesema daraja hilo la kudumu limejengwa kwa gharama ya shi. milioni 527 na mkandarasi mzawa wa kampuni ya Byam kutoka Jijini Dar es Salaam.

“Daraja hili la mto Nkala ni daraja ambalo kwa watu wa Momba upande wa Chitete, limesaidia sana kwani kuna jumla ya vifo saba viliripotiwa kutokea wakati kukiwa na daraja dogo na baada ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutupatia fedha na tumefanikiwa kujenga daraja kubwa na la kudumu, ambalo sasa limemaliza changamoto zote za usafirishaji, ikiwemo madhara kama vifo,” amesema Mhandisi Bishanga.

Amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 87.4 ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao ya mpunga na kwenda kwenye masoko yaliyopo katika miji ya Mlowo na Tunduma.