August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAHA yabuni teknolojia mpya za bustani za nyumbani

Na Mwandishi wetu, Timesmajiraonline,Arusha

TAASISI ya Kilimo cha Mboga, Matunda na Viungo Tanzania (TAHA) imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya bustani za nyumbani na jikoni kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuzalisha mazao ya viungo na mimea tiba (herbs) hata katika maeneo madogo yanayozunguka makazi yao.

Akizungumza kuhusu teknolojia hiyo, Agosti 7,2026 Mtaalamu wa Lishe kutoka TAHA, Innocent Mbwando, alisema mpango huo unalenga kuhakikisha familia nyingi zinapata fursa ya kuzalisha mazao yenye virutubisho muhimu pamoja na mimea tiba kwa matumizi ya kila siku bila kuhitaji eneo kubwa la kilimo.

Mbwando amesema teknolojia hiyo inawasaidia watumiaji wa mazao ya herbs kujenga utamaduni wa kutumia mimea yenye manufaa kwa afya, huku baadhi ya mimea hiyo ikiwa na uwezo wa kusaidia kujikinga na magonjwa mbalimbali pale inapotumika kama sehemu ya lishe bora.

Amefafanua kuwa pamoja na manufaa ya kiafya, bustani hizo zinawapa wananchi nafasi ya kupata mazao safi na salama muda wote, hivyo kupunguza gharama za kununua viungo na herbs kutoka sokoni.

Aidha, aliwahimiza wakulima na wananchi kwa ujumla kuzingatia kilimo cha viungo na herbs kwa kutumia teknolojia hiyo, akieleza kuwa mazao hayo yana thamani kubwa na yanazidi kuhitajika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mbwando amesema TAHA inaendelea kuboresha teknolojia hiyo na kuongeza juhudi za kuitangaza kwa wananchi wengi zaidi ili watu wengi wanufaike na fursa za lishe, afya pamoja na biashara zinazotokana na mazao hayo.

Ameongeza kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa herbs kutachangia kuboresha usalama wa chakula na lishe, kuongeza kipato cha kaya na kufungua fursa mpya za ajira kupitia mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga, viungo na mimea tiba.

Akihitimisha, Mbwando alitoa wito kwa jamii kuanzisha bustani za nyumbani na jikoni na kutumia mazao ya herbs kama sehemu ya lishe ya kila siku, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha afya za wananchi, kuimarisha kinga ya mwili na kuongeza ustawi wa familia pamoja na uchumi wa taifa.