Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
MKURUGENZI wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule, amewataka wananchi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara kuacha tabia ya kuchimba visima vya maji kiholela bila kufuata taratibu na kupata vibali vinavyotakiwa.
Segule amesema hayo leo Agosti 8,2026 hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Themi jijini Arusha, ambapo bodi hiyo inashiriki kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi na uhifadhi wa rasilimali za maji.
Amesema uchimbaji wa visima bila kufuata taratibu unaweza kusababisha madhara makubwa kwa mazingira pamoja na kuathiri upatikanaji na usalama wa maji kwa watumiaji mbalimbali.
Segule ameeleza kuwa baadhi ya wananchi wanaochimba visima bila kufanya uchunguzi na kufuata taratibu za kitaalamu wanaweza kujikuta wakitumia maji ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu, hali inayoweza kuhatarisha afya za watumiaji.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi wanaohitaji kuchimba visima kuhakikisha wanapata vibali husika kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani na kufuata taratibu zote zinazotakiwa kabla ya kuanza kazi hiyo.
Aidha, Segule aliwataka wananchi kushirikiana katika kulinda vyanzo vya maji na kutoa taarifa mara moja kwa bodi hiyo endapo watabaini mtu au taasisi inayokiuka sheria na kanuni za uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji, huku akisisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Segule amesema Bodi ya Maji Bonde la Pangani itaendelea kushiriki katika maonesho mbalimbali, ikiwemo Nane Nane, kwa lengo la kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu kuhusu matumizi sahihi ya maji, uchimbaji wa visima kwa kufuata taratibu pamoja na namna ya kulinda vyanzo vya maji.


More Stories
Nanauka ametaka TADB kushirikiana kuwasaidia vijana
TAHA yabuni teknolojia mpya za bustani za nyumbani
Wakulima zaidi ya 200 wapatiwa elimu matumizi ya viuatilifu