April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TADB, TCB kushirikiana utoaji mikopo kwa wakulima

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kupitia Mfuko wake wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS), imekubaliana na Benki ya Biashara Tanzania (TCB), kuongeza mkataba kwa ajili ya kutoa dhamana ya mikopo ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.

Mkataba huo wa pande zote mbili utaiwezesha benki ya TADB, kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kupitia TCB, ambapo watatoa mikopo kwenye mnyororo ya thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Kwa upande wa TADB, yenyewe itatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hususani kwa vijana, wanawake na miradi inayosaidia kupunguza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla fupi ya utiaji saini leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege amewapongeza TCB kwa kazi nzuri wanayofanya kwa kuona umuhimu wa kuendelea kuchangia maendeleo ya kilimo nchini kupitia matawi yao.

Amesema, Mkataba huo utaiwezesha TCB kuongeza wigo wa utaoaji mikopo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hasa kwa wanawake na vijana.

“Nawapongeza kwa kuona umuhimu wa kuendelea kutoa mikopo kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi naamini mkataba huu mpya baina yetu.

“Utasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo na itakuwa raihisi kuwafikia kwa wingi zaidi hususani wale waliopo pembezoni mwa miji, mikoa na wilaya,” amesema Nyabundege.

Hata hivyo amesema, ushirikiano wa TADB na TCB ulianza Mei, 2018 umekuwa wenye tija na manufaa makubwa kwa wakulima na sekta ya kilimo nchini.

Nyabundege amesema, mpaka mkataba huo wa awali umemalizika tayari TCB, kupitia dhamana ya TADB imeshatoa mikopo yenye jumla ya shilingi. Bilioni 34.1 kwa wanufaika wa moja kwa moja 2,638 na wanufaika wasio moja kwa moja zaidi ya 7,750.

Amesema, zaidi ya asilimia 95 ya wanufaika ni wakulima wadogo na wajasiriamali wadogo wa vijijini wanaoshughurika na mnyororo wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Pia, amesema jumla ya shilingi bilioni 4.3 zilitolewa kwa wanawake 448 na shilingi bilioni 3.4 zilitolewa kwa vijana 416 katika mikoa, wilaya mbalimbali nchini.

Aidha, amesema ili kuongeza wigo kwa TCB kutoa mikopo zaidi, TADB imefanya maboresho na imeongeza kiwango cha dhamana kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 70 kwa miradi ya wanawake, vijana na miradi inayosaidia kupunguza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TADB, kutimiza majukumu yake huku akitoa wito kwa benki na taasisi za kifedha kutoa ushirikiano kupitia mfuko wa dhamana wa wakulima wadogo (SCGS).

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo amesema wamefikia uwamuzi wa kuongeza mkataba na TADB kutokana na faida walizozipata.

“Tunaishukuru TADB, kwa kutuingezea nguvu kwa ajili ya kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvu wengi zaidi.

“Nia ya kuongeza mkataba huu kuhakikisha tunawafikia wakulima wa pande zote za nchi kwa kuwaongezea mitaji kwa riba nafuu itakayowezesha kufanya kilimo cha kibiashara ili kujikwamua kiuchumi baina yao na nchi kwa ujumla,” amesema Mihayo.