April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shule kufungwa yageuka changamoto Mwanza

Judith Ferdinand, Mwanza

Baada ya Serikali kusitisha masoma kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi aina ya corona nchini, ili kuwaepusha wanafunzi na maambukizi ya ugonjwa huo Mkoani Mwanza kumeibuka changamoto ya watoto kurandaranda sokoni.

Hii ni kutokana na baadhi  ya wazazi  Mkoani humo kikiuka maagizo  yaliyotolewa na  Serikali ambapo wamekuwa na tabia ya kuwatumia watoto wao kufanya biashara katika maeneo ya mikusanyiko ikiwemo sokoni.

Akizungumza jana Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji  elimu kwa wananchi wote  wa Mkoa huo, wa namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo,ambalo  litaendeshwa na Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mongella,alisema baada ya Rais kuelekeza taasisi za elimu zifungwe na watoto wakae nyumbani  ili kuwanusuru na maambukizi ya ugonjwa huo bado wanawashuhudia  watoto wakirandaranda mitaani jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.

“Corona ni hatari na  inaua hivyo wananchi wanapaswa kutoleta mzaha bali kulipa kipaumbele suala  hilo na kulichukulia kwa umakini kwa  kuzingatia maelekezo yanatokewa na wataalamu wa afya,hivyo kwa wazazi ambao wataendelea kuwatumia watoto katika mikusanyiko kipindi cha gonjwa hili hatua kali dhidi yao zitachukuliwa,” alisema Mongella.

Sanjari na hayo,aliwataka wazazi kutambua  kuwa watoto hawajafunga shule bali wapo nyumbani ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huo,hivyo wasitumie nafasi hiyo kuwafanyisha kazi zinazowafanya kuzurura mitaani na badala yake wanapaswa kukaa nyumbani mpaka hali itakapokuwa sawa.

“Vyombo vya ulinzi na usalama,RPC yupo hapa kwa niaba ya wenzake jeshini,Polisi na Mshauri wa migambo tuwaambie watu wetu wote kwa nguvu zote tutawanyike kila mtu atumie muda wowote anaoupata kutoa elimu na kuhamasisha kama Rais alivyotuelekeza tupambane na janga hili,”alisema Mongella.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Red Cross Mkoa wa Mwanza Salome Tuppa,alisema lengo ni kuwafikia wananchi wote waliopo katika Mkoa huu na kuwapatia elimu hiyo ili wawe na utayari wa kupambana na virusi hivyo .

” Tutaenda kila mahali hata vijijini kutoa elimu na sehemu ambako gari hazitafika tutatumia pikipiki ili kuifikisha elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza,” alisema Tuppa.

Naye Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mwanza Mhadisi Karonda Hassan,aliiomba serikali kuwapatia vipimo kwa ajili ya kupima dalili za ugonjwa huo katika kivuko cha   Kigongo Ferry na Busisi kwa kuwa eneo hilo linapokea na kuvusha watu wengi kwa siku.

” Kila mtu akifika lazima anawe mikono lakini ni vyema tukapatiwa na vipimo vya joto kwani uwezekano upo mtu anaweza kuja hapa akiwa ni muathirika wa ugonjwa huo na tusimtambue na akanawa mikono na kuchangamana na wasafiri wengine hapa lazima ataeneza ugonjwa hu, ” alisema Hassan.

Aidha Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini Yassini Ally  akizungumzia adha hiyo ya watoto kuzagaa mitaani,alisema iwekwe marufuku kwa wazazi wanaoingia sokoni kutoambatana na watoto na suala hilo liwe ni zoezi endelevu litakalo fanyika huku wakiwataka wazazi wenye tabia ya kuwaleta kwenye biashara ama kuwaruhusu watoto kwenda kwenye mikusanyiko waache bali watambue uthamani wa watoto wao.

“Tuwe na oparesheni madhubuti zinazoangazia usiku na mchana kwa sababu tunawaona watoto wakizagaa kwenye maeneo ya club,bar na masoko jambo ambalo ni hatari hivyo hatua zichukuliwe ili kuwanusuru watoto wasije kupata maambukizi,”alisema Ally.

Mongella alifanya ziara ya kukagua na kujionea utayari wa taasisi kupambana na kuenea kwa virusi hivyo katika maeneo ya Kigongo Ferry na Busisi,Stend ya mabasi Nyabulogoya, soko la Mirongo na soko la Mbugani ambapo kila sehemu walizingatia maelekezo yanayotolewa na idara ya afya.