May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shamin Mwasha, mumewe wakutwa na kesi ya kujibu

 Na Grace Gurisha, TimesMajira Online, Dsm

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Kifisadi), imemkuta na kesi ya kujibu Mfanyabiashara Abdul Nsembo na Mkewe Shamim Mwasha (Pichani juu) wanaokabiliwa na mashtaka ya kukutwa na dawa za kulevya.

Aidha, mahakama hiyo imesema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi nane pamoja na vielelezo sita ili kuthibitisha mashtaka hayo.

Jaji Elieza Luvanda, amesema Mahakama baada kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, umeona washtakiwa Nsembo na Shamimu wana kesi ya kujibu.

Kesi hiyo imepangwa Septemba 3, mwaka huu kwa washtakiwa hao kuanza kujitetea ambapo walidai watakuwa na mashahidi watatu, ikiwamo wao wenyewe.

Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Veronica Matikila.

 Vielelezo  vilivyoambatanishwa kwenye kesi hiyo  ni maelezo ya onyo kwa washtakiwa wote wawili, hati ya ukamataji, ripoti ya uchunguzi wa maabara ya Serikali, fomu ya kuwasilisha sampuli maabara, taarifa ya usajili wa gari kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na bahasha zilizokuwa na dawa za kulevya.

Katika maelezo ya shahidi wa kwanza ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Paschal Daudi ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa upekuzi alidai kuwa Mei Mosi, 2019 alipewa kazi ya kuongoza ukaguzi katika nyumba ya mfanyabiashara  Nsembo iliyopo Mbezi beach wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alidai kuwa kwa mujibu wa maelezo ya Daudi walifika eneo la tukio muda wa saa 2 usiku na kugonga geti ambalo lilifunguliwa na mlinzi aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Senkokwa na baada ya kujitambulisha na kumueleza kilichowapeleka Senkokwa, aliwaeleza wasubiri amuite mwenye nyumba ambaye ndiye mwenye ufunguo.

Kwa mujibu wa maelezo hayo baada ya muda mfupi alitoka mama ambaye alijitambulisha kwa jina la Shamim Mwasha ambaye alikiri kuwa ndiye mama mwenye nyumba na mke wa Nsembo.

Inadaiwa Shamim alipoulizwa kuhusu mume wake, alidai hajui alipo kwani walikuwa na ugonvi wa kifamilia na hajui angerudi muda gani, lakini wao walimuomba awaruhusu wafanye ukaguzi naye akawaruhusu.

“Kabla ya ukaguzi walimruhusu Shamim awakague, alifanya hivyo na kujiridhisha kwamba hawakuwa wamebeba kitu chochote hatarishi kwake.

Walipofanya ukaguzi katika maeneo kadhaa hawakufanikiwa kupata chochote wala kumuona yeyote mpaka walipoingia katika moja ya chumba na kukuta vipande vya Gypsum vikiwa vimeanguka na alama ya mguu ikionesha wazi kuwa kuna mtu alipanda darini muda mfupi uliopita,” alidai.

Alidai alimwagiza mmoja wa askari alioongozana nao aliyemtambulisha kwa jina la Brown apande darini kuangalia kama kuna mtu lakini hakuona mtu, baada ya kurudi mara ya pili aligundua kulikuwa na mfuniko unaotokea upande wa nje kwa kupitia kwenye paa hivyo aliufunua na kutoka nje kwenye kibaraza cha kuwekea tanki la maji ambalo Nsembo alikuwa amejificha nyuma yake.

Inadaiwa kuwa Brown alimshusha Nsembo chini na kuendelea na upekuzi ambapo walifanikiwa kukamata vitu kadhaa ikiwemo pasi ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa cha Nsembo, vifaa mbalimbali vya mawasiliano kama simu, kifaa cha kuhifadhia picha za cctv, na kifaa cha kuhifadhia nyaraka za kompyuta (external backup).

Mbali na vifaa hivyo walikuta pia vikopo vinne vyenye unga ambao baadaye ulibainika kuwa ni dawa za kulevya na waliendelea na upekuzi katika magari ambapo katika gari moja aina ya Landrover Discovery lenye namba T 817 BQN nyuma ya kiti walikuta mfuko wa kitambaa uliowekwa kwenye mfuko laini wenye unga ambao baadaye ulibainika kuwa ni dawa za kulevya.

Alidai waliweka kumbukumbu ya vielelezo vyote na katika fomu maalumu na kuwekaka saini na wahusika wote wakiwemo washtakiwa.

Maelezo hayo pia yalithibitishwa na maelezo ya mashahidi wegine 11 waliobaki ambao maelezo yao yalishabihiana na maelezo ya Daudi.

Shamimu ambaye ni mmiliki wa Blog 8020 Fashion na mumewe wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019, ambayo ni kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70