May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakabidhi vifaa tiba vya milioni .100/- Kituo cha Afya Magazini

Na Cresensia Kapinga, TimesimajiraOnline, Namtumbo

BOHARI ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba vya kisasa vya upasuaji kwa Kituo cha Afya cha Magazini kilichopo Kata ya Magazini Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma vyenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 100.

Vifaa hivyo vinalenga kuwezesha kituo hicho kuimarisha huduma za afya kwa watu wenye magonjwa mbalimbali hasa yanayohitaji upasuaji.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa tiba hivyo jana, Meneja wa MSD Kanda ya Iringa, Robart Rugembe, amesema kuwa vifaa hivyo vitasaidia watu wengi ambao kwa sasa baadhi yao walikuwa wakisumbuliwa na magonjwa yanayohitaji upasuaji ikiwemo akina mama wajawazito.

Rugembe amesema bado watapeleka vifaa tiba vya kisasa vingine vyenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 100 kwenye kituo hicho, hadi pale kituo hicho kitakaposheheni vifaa vya kutosha kwa ajili ya kutoa huduma bora.

“Nilikuwa naangalia hapa nikasema katika hii migao inayoendelea hamna jenereta, lakini hapa jenereta inahitajika sana, kwa hiyo MSD tutaleta jenereta ambayo itasaidia shughuli za upasuaji,” amesema Rugembe.

Ameviitaja baadhi ya vifaa vilivyopelekwa kwenye kituo hicho kuwa ni kitanda maalum cha kufanyia upasuaji, taa ambayo inatoa mwanga wakati wa upasuaji, vifaa vya uchunguzi, mashine ya kutakasa vifaa, vifaa vya kufulia nguzo na vifaa vya kukaushia vyombo, pamoja na mashine za upasuaji za kutosha.

Awali akipokea msaada huo, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Magazini, Dkt.Rashid Athuman amesema kituo hicho tangu kianze kufanya kazi hakijawahi kutoa huduma za upasuaji.

“Lakini kwa sasa vifaa tiba hivi vitasaidia kutumia teknolojia ya kisasa zaidi ambayo itamfanya mgonjwa kurejea afya yake kwa haraka zaidi,” amesema Dkt. Athuman.

Dkt. Athuman amesema kituo hicho kina malengo na mikakati ya kuhakikisha kinatoa huduma bora ambazo wananchi wenye kipato duni wanaweza kuzifikia na kuzimudu na si vinginevyo.

Baadhi ya wananchi wa kata ya magazeti waliojitokeza kuhushuhudia makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwa ajili ya kifuatilia makabidhiano ya vifaa tiba Kituo cha Afya cha Magazini kilichopo Kata ya Magazini Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wakifuatilia hafla ya makabidhiano hayo.

“Tunatoa shukrani zetu kwa Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa ushirikiano tunaopewa na MSD tunaomba ushirikiano huu uendelee kudumishwa kwa mtazamo wa kwamba lengo letu ni moja, na wajibu wetu ni mmoja, ni kwa ajili ya kuhudumia wananchi hasa hawa waliopo mipakani na nchi jirani ya Msumbiji,” amesema Dkt. Athuman.

Awali akisoma taarifa fupi ya kituo hicho cha afya Mtendaji wa Kata ya Magazini, Mussa Ponera alisema kituo hicho kilianza kujengwa 2019/2020 ambapo walipokea fedha kutoka Serikali Kuu vya kiasi cha sh. Milioni 500 .

Amesema hadi sasa wanahitaji kiasi cha sh. milioni 120 ili kukamilisha miundombinu ya vyoo, mahabara, jengo la upasuaji pamoja na jengo la mama na mtoto.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa lengo na mikakati ya kuhakikisha kwamba inatoa huduma bora ambazo wananchi wenye kipato duni wanaweza kuzifikia na kuzimudu.

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vita Kawawa, akihutubia wananchi wakati wa mapokezi ya vifaa tiba, Katika Kata ya Magazini, wilayani Namtumbo kwa ajili ya Kituo cha Afya Magazini.

Amesema zoezi la kugawa vifaa tiba kutoka MSD litaendelea kufanyika ili kufikia lengo la kutoa huduma iliyokuwa bora zaidi kwa wagonjwa na kuondokana na wimbi kubwa la baadhi ya wagonjwa kwenda umbali mrefu kutibiwa kwa ukosefu wa baadhi ya vifaa kwenye vituo vya afya vilivyopo Jimbo la Namtumbo.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Magazini, Gress Kapinga, alisema vifaa tiba hivyo vitawasaidia kuondokana kutembea umbali wa kilometa 202 kwenda kufuata huduma za upasuaji Hospital ya Mkoa Songea (HOMSO).

Amesema kutokana na hali hiyo wajawazito wengi wamepoteza maisha kwa kukosa huduma za upasuaji.

Kwa upande wao wananchi wa kata hiyo wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa tiba hivyo, kwani walikuwa wanapata shida kwa kukosekana kwa vifaa vya upasuaji katika kituo hicho.

Pamoja na kupelekwa vifaa hivyo, waliiomba Serikali kuwaharakishia huduma ya umeme katika kituo hicho ili vifaa hivyo viweze kutumika kama ilivyokusudiwa.