May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jiji la Mwanza lapata mlipuko wa kipindupindu,wananchi watakiwa kuchukua tahadhari

Judith Ferdinand, Mwanza

Halmashauri ya Jiji la Mwanza limekubwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu baada ya kubaini wagonjwa saba ambao wamekutwa na ugonjwa huo baada ya kuchukuliwa sampuli.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi ya Halmashauri hiyo kilichofanyika Januari 9,2024,Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Dkt.Sebastian Pima ameeleza kuwa Januari 4 mwaka huu walipokea watu wawili waliokuwa na dalili za ugonjwa wa kipindupindu ambao walitokea Mkoa wa Simiyu.

“Wanavyosema wao ni sehemu ambayo wanachukulia mizigo,wakiwa wanarudi walipofika Mwanza moja kwa moja walienda kwenye kituo chetu cha afya Igoma na walipofika tukawaona wanadalili ya ugonjwa wa kipindupindu tukachukua sampuli na tulipo pima tulibaini kuwa wana ugonjwa huo na mara moja tuliwapeleka kwenye kituo chetu cha Mkuyuni,” ameeleza Dkt.Pima.

Dkt Pima ameeleza kuwa baada ya hapo walifuatilia wamzz schetokea maeneo gani na kujua kuwa wametokea eneo la Kakebe Kata ya Igoma ndani ya Jiji la Mwanza.

Baada ya visa hivyo viwili viliendelea kutokea visa vingine eneo la Mkolani visa viwili lakini visa vitatu vinatokea Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

“Hadi sasa tangu Januari 4 mwaka huu tulipo pata mlipuko wa kipindupindu tumeisha pata wagonjwa saba ambao walilazwa ambapo wawili wa awali tumeisha waruhusu hali zao zinaendelea vizuri na kwenye kituo chetu cha matibabu kwa sasa tuna wagonjwa watano ambao wanaendelea na matibabu na wanaendelea vizuri,” ameeleza Dkt.Pima.

Aidha mpaka sasa wamefanya ufuatiliaji kwa familia waliokutana na wagonjwa kwa watu 18 ambao mpaka sasa hawajaonesha dalili za ugonjwa huo ambapo wanaendelea na kuwabaini wengine zaidi kwani wagonjwa hao wamekutana na watu wengi tofauti tofauti.

“Kwa ambao wataonekana na dalili tutawachukua sampuli na wakithibitika kuwa na ugonjwa tutawachukua kwa ajili ya kuanza kuwapa matibabu

Haya hivyo ameeleza kuwa ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia ya kula chakula,kunywa maji au kitu chochote kilichokutana na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu na mara nyingi unakuwa na mchanganyiko wa kinyesi chenywe vimelea.

“Hivyo tunahamasisha jamii kunawa mikono kwa maji safi yanayo tiririka na sabuni wakati wote akitoka kujisaidia,akitaka kula chochote,wakati wote wale chakula cha moto na kuepuka kula chakula kilicho poa,kunywa maji yaliochemshwa au kutibiwa kwa kuwekewa dawa,”ameeleza Dkt.Pima.

Pia ameeleza kuwa ni rahisi kuepuka na kujikinga na ugonjwa huu kama watazingatia kanuni za afya ikiwemo matumizi sahihi ya vyoo muda wote sababu kujisaidia ovyo ovyo unakuwa unasambaza wadudu hivyo kusababisha maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana Thomas Salala kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo,ametaka katika maeneo ya shule,taasisi na masoko kuwe na wataalamu maalumu ambao wataenda katika maeneo hayo ili kutoa elimu na kudhibiti uchagu kwa kuhakikisha kunakuwa na vitu vya kuweka taka na maji yanapatikana ili kuikinga jamii na mlipuko wa ugonjwa huo.

Pia kusimamia matumizi ya vyoo,uuzaji wa vyakula holela udhibitiwe pamoja na uuzaji wa vyakula maeneo yasiyo rasmi pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha ili iweze kuzingatia usafi na kanuni za afya.

“Eneo la Buhongwa linapaswa kuangaliwa kwa umakini na kuhakikisha pamoja na kufanya biashara ila pawe na utaratibu wa usafi kwani tusipo dhibithi ukanda huo ambao una muingiliano mkubwa wa watu pamoja na shule ambazo zimezunguka tutapata madhara makubwa,”kuwe na vitu vya kuweka taka na maji pia usiku.

Naye Ofisa Usafi na Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle, mkakati walionao kwa upande wa mazingira wa kuhakikisha mazingira yote yanaimarishwa ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa kushirikiana na vikundi au kampuni za usafi katika Halmashauri ya Jiji hilo.

“Halmashauri ya Jiji la Mwanza ina kitengo cha Askari lakini kwa kushirikiana na Askari wa Jeshi la Akiba kwa ajili ya kuhakikisha wanadhibiti uchafuzi wa mazingira na wote wanaofanya biashara katika maeneo ambayo siyo rasmi,hivyo natoa rai kwa waliorudi kufanya biashara kwenye maeneo ambayo siyo rasmi warudi katika maeneo yao rasmi,”ameeleza.

Pia ametoa rai kwa wananchi kuacha tabia mbaya ya kununua vyakula katika maeneo ambayo siyo rasmi na kila mmoja atimize wajibu wake.

Mwenyekiti wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWS) Nyamagana Yohana Wanga ameshauri nguvu zielekezwe shuleni kwa wanafunzi ambao wapo mama ntilie wanawauzia chakula pia taarifa hiyo iwafikie wananchi kwa haraka kwa sababu ni dharura ili wachukue hatua za kujikinga na ugonjwa huo.