April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SADC kupeleka jeshi Cabo Delgado

MAPUTO, Viongozi wa Jumuiya ya Maedeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekubali kupeleka wanajeshi kusaidia kudhibiti uasi unaofanywa na kikundi cha wanamgambo wa Kiislam kinachofanya mauaji na kusababisha taharuki Kaskazini mwa Msumbiji kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Stergomena Tax baada ya kikao cha dharura kilichofanyika mjini Maputo nchini Msumbiji.

“SADC imeidhinisha kupelekwa kikosi cha dharura kuisaidia Msumbiji kupambana na ugaidi na vitendo vya uhalifu unaotokana na misimamo mikali huko Cabo Delgado,”amesema Tax.

Aidha, licha ya Katibu Mtendaji kutoa taarifa hiyo hakufafanua ukubwa wa kikosi hicho na muda wa kuwasili nchini Msumbiji.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe.

Akihutubia katika mkutano Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi amesema,wanatambua na kuridhia mshikamano na msaada wa nchi wanachama wa SADC na nchi rafiki ambao wanaunga juhudi kuzuia ugaidi kupata sehemu mwafaka kuendesha mashambulizi katika nchi na kanda zima.

Waraka uliopatikana kwa siri mapema mwaka 2021 ulikuwa unapendekeza kupelekwa takribani wanajeshi 3,000 katika mkoa wa Cabo Delgado, ambapo waasi wameviteka vijiji na miji kadhaa na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Ghasia zimeongezeka katika sehemu za Kaskazini mwa Msumbiji lenye utajiri wa gesi uliopatikana mwishoni mwa 2017 na kuna wasiwasi zinaweza kuenea katika nchi jirani.

Machi 24,mwaka huu wanamgambo wenye uhusiano na kikundi cha Islamic State walianzisha mashambulizi mbalimbali yaliyopangwa kufanyika wakati mmoja katika mji wa Kaskazini wa Palma, ikiharibu majengo na kuua wakazi huku maelfu yao wakikimbilia msituni.

Aidha, mashambulizi yamefikia kuongezeka kwa uvunjifu wa amani na kusababisha watu takriban 800,000 kukimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 2,800 ambapo nusu yao ni raia.