April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makamu wa Rais ziarani Ufaransa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa kundi la maseneta wa Kifaransa marafiki wa Tanzania, Ronan Dantec.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika jengo la Bunge la Seneti, Paris nchini Ufaransa.Seneta Dantec amezungumza na Makamu wa Rais juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira lengo likiwa ni kupunguza hewa ukaa duniani. Pia ameshauri uwepo wa mfuko wa fidia kwa wale watakaothirika na masuala ya kuhifadhi na kulinda mazingira.

Makamu wa Rais amesema, amefurahishwa na namna uhifadhi wa mazingira unavyofanyika nchini Ufaransa ikiwemo Mji wa Paris licha ya ukongwe wa mji huo.

Amemuhakikishia Seneta Dantec kwamba, Tanzania ipo tayari kushirikiana na Ufaransa katika uhifadhi wa mazingira na kuwakaribisha Maseneta rafiki wa Tanzania katika kutekeleza hilo kwa pamoja.

Amesema, Tanzania inazingatia uhifadhi wa mazingira, lakini kwa kulinda haki za wananchi wakati wa utekelezaji wa uhifadhi huo.

Pia Makamu wa Rais ametembelea maktaba iliyopo katika jengo hilo na kujionea historia mbalimbali iliyohifadhiwa vizuri ya uongozi mbalimbali uliowahi kutawala nchi ya Ufaransa.

Aidha, Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango ametembelea ukumbi wa Mikutano ya Bunge la Seneti na kupokea maelezo kutoka kwa Maryam Zadeh mmoja wa wahudumu katika Bunge hilo.

Makamu wa Rais yuko nchini Ufaransa kuhudhuria Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (Generation Equality Forum) linalofanyika Juni 30 hadi Julai 2 ,2021 lenye lengo la kuchagiza haki za usawa wa kijinsia kama zilivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing wa mwaka 1995.