June 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airtel,Serikali waungana kupanda miti Bagamoyo na kusafisha fukwe Dar


Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imetoa wito kwa wadau wa maendeleo kuimarisha ushirikiano na serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu na kuendeleza uhifadhi wa mazingira shuleni ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.


Wito huo ulitolewa Alhamisi wakati wa zoezi la kupanda miti lililoandaliwa na Airtel Tanzania chini ya udhamini wa Airtel Africa Foundation katika Shule ya Msingi Kiromo iliyopo Wilayani Bagamoyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.


Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu wa Wilaya ya Bagamoyo, Hamis Kimenya ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo ameiipongeza Airtel Tanzania kwa kushirikia na Airtel Africa Foundation kwa kuendelea kuisaidia Shule ya Msingi Kiromo na kuwahimiza wadau wengine wa sekta binafsi kujiunga na juhudi hizo zinazolenga kuboresha elimu na kulinda mazingira.


Amesema juhudi za uhifadhi wa mazingira, hasa upandaji miti, zinachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maeneo ya shule, kuongeza uoto wa kijani, kutoa kivuli, na kutengeneza mazingira yenye afya na yanayofaa zaidi kwa ujifunzaji.


“Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inaendelea kujitolea kuweka mazingira wezeshi ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi, hasa katika sekta ya elimu. Tunahimiza wadau wengi zaidi kuunga mkono shule na jitihada za uhifadhi wa mazingira,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, amesema Siku ya Mazingira Duniani inakumbusha ulimwengu kuwa ulinzi wa mazingira ni jukumu la pamoja linalohitaji hatua za pamoja kutoka kwa serikali, taasisi binafsi na jamii.


Amesema mpango wa kampuni hiyo wa kupanda miti katika Shule ya Msingi Kiromo unaonyesha dhamira yake ya muda mrefu katika uendelevu wa mazingira na maendeleo ya jamii.


“Leo hatupandi miti tu; tunawekeza katika mazingira yetu, jamii zetu, na vizazi vyajavyo,” alisema Kamoto. “Miti hii ya matunda itasaidia kulinda ardhi, kuboresha ubora wa hewa, kutoa kivuli, na baadaye kutoa matunda yatakayowanufaisha wanafunzi na jamii inayozunguka.”


Kamoto ameongeza kuwa mpango huo unaenda sambamba na maono ya Taasisi ya Airtel Africa (Airtel Africa Foundation) kupitia mpango wake wa “Adopt a School”, (Shule Yetu) ambao unasaidia uendelezaji wa mazingira salama, ya kijani, jumuishi na wezeshi ya kujifunzia kwa watoto kote Afrika.


Amebainisha kuwa Airtel imeendelea kuongeza juhudi za uhifadhi wa mazingira, akigusia kuwa mwaka jana kampuni hiyo ilifanya zoezi la kusafisha fukwe katika Fukwe ya Kawe jijini Dar es Salaam.Mwaka huu, Airtel Tanzania imepanua juhudi zake kupitia upandaji miti katika Shule ya Msingi Kiromo, ikionyesha kuongezeka kwa dhamira ya uendelevu.


Katika hatua nyingine, mnamo Juni 5, 2026, Airtel pia ilifanya zoezi kubwa la kusafisha fukwe katika fukwe za Msasani na Kawe jijini Dar es Salaam kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. Zoezi hilo lilisimamiwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).


Akizungumza wakati wa usafi huo, Afisa Mazingira wa NEMC, Felician Kairuki amewasihi wadau kuimarisha ushirikiano katika ulinzi wa mazingira kulingana na sera za kitaifa na mikakati ya usimamizi wa mazingira.


“Tunasisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wadau wote ili kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Kairuki.


Ameongeza kuwa ushirikiano endelevu kati ya taasisi za serikali, wadau wa sekta binafsi na jamii ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za mazingira kama vile uchafuzi wa mazingira na usimamizi wa taka.


Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma Airtel Tanzania, Jackson Mbando amesema kampuni hiyo imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya uendelevu, ikiwa ni pamoja na kukuza suluhisho za kidijitali zinazopunguza utegemezi wa karatasi na vifaa vingine vinavyoweza kuchangia uharibifu wa mazingira.


Amesema hatua hizi ni sehemu ya dhamira pana ya Airtel ya kufanya biashara kwa masuala ya uwajibikaji na usimamizi wa mazingira.


Afisa Mtendaji wa Kata ya Kawe, Husna Nondo ameipongeza Airtel kwa kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya kusafisha fukwe, akibainisha kuwa mamlaka za serikali za mitaa zinaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu binafsi na taasisi zinazochafua mazingira.


Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na jamii ni muhimu katika kuhakikisha kuwa fukwe, maeneo ya wazi na mazingira ya mijini yanabaki kuwa safi, salama na endelevu.

Mipango hiyo ya pamoja huko Bagamoyo na Dar es Salaam inaangazia ukuaji wa ushirikiano kati ya sekta binafsi, mashirika ya serikali na vyombo vya udhibiti katika kuendeleza uhifadhi wa mazingira, kukuza uendelevu na kuboresha ustawi wa jamii kote nchini Tanzania.