May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Njaa kali yatua Tigray

TIGRAY, Umoja wa Mataifa umetaka kuwa na fursa isiyo na vikwazo vyovyote ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu jimboni Tigray nchini Ethiopia.

Sambamba na kukoma kabisa kwa mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wanaosambaza misaada hiyo ili wenye uhitaji wa haraka waweze kupatiwa chakula.

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA), Ramesh Rajasingham wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwa ni kikao cha kwanza cha wazi cha baraza hilo kuhusu mgogoro unaondelea Kaskazini mwa Ethiopia.

Hotuba ya afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ilitoa taswira mbaya jimboni Tigray ikionesha kuwa watu 400,000 wamevuka hata kile kiwango cha kawaida cha njaa na wengine milioni 1.8 wako hatarini kujiunga nao.

“Takribani watu milioni 1.7 wamepoteza makazi kutokana na mapigano jimboni Tigray kati ya vikosi vya serikali na kikosi cha ulinzi wa Tigray ambapo 60,000 kati yao wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Sudan,”amesema Rosemary DiCarlo Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya siasa na ujenzi wa amani.

DiCarlo amesema, matukio mengine zaidi ya 1,200 ya ukatili wa kingono na kijinsia yameripotiwa, idadi ambayo amesema inaweza kuwa kidogo tu ya matukio halisi katika mzozo huo ambao unaathiri zaidi wanawake na watoto.

“Maisha ya idadi kubwa ya wananchi wa Tigray yanategemea uwezo wetu wa kuwafikishia chakula, dawa, vvyakula vyenye virutubisho na misaada mingine ya kibinadamu,”amesema Kaimu Mkuu huyo wa OCHA akiwajulisha wajumbe 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kutokana na hali hiyo amesema, wanahitaji kuwafikia wananchi hao kwa haraka, hivyo akatoa wito wa kuweza kuwafikishia misaada bila vikwazo vyovoyte.

“Nikimaanisha kuwa sheria ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu lazima izingatiwe na makundi yote yanayopigana ili tuweze kufikisha misaada bila vikwazo,”amesema.

Mkutano wa Ijumaa ulikuwa mkutano wa kwanza wa wazi kabisa tangu mzozo wa Tigray uanze miezi minane iliyopita, ijapokuwa baraza hilo limeshakuwa na vikao 6 na mijadala lakini ya faragha.

Mkutano huo ulifanyika siku nne baada ya Ethiopia kutangaa sitisho la mapigano kwa ajili ya kupitisha misaada ya kibinadamu, sitisho ambalo hata hivyo jeshi la ulinzi la Tigray ambalo linadhibiti mji mkuu wa jimbo hilo Mekele na miji mingine halikukubaliana nalo.

Rajasingham alitumia kikao hicho kutaka kukoma kwa mapigano ili misaada ipitishwe bila vikwazo vyovyote.