June 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mbarali apongeza utendaji wa Mweli

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI wilayani Mbarali mkoani Mbeya imempongeza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Raymond Mweli, kwa jitihada zake za kujituma katika kazi na kutekeleza maelekezo ya serikali kwa ufanisi.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Maulidi Surumbu, wakati akitoa salamu za serikali katika hafla ya utoaji wa mikopo kwa vikundi 52 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Surumbu amesema halmashauri ya Mbarali imeendelea kufanya vizuri kutokana na utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa kwa mkurugenzi huyo, huku akiwataka watumishi kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo, ushirikiano wa watumishi utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma na kutatua kero za wananchi kwa wakati.

Kwa upande wake, Bahati Ndingo amesema anatambua mchango wa Mweli katika kusimamia maendeleo ya halmashauri, akibainisha kuwa vikundi vingi zaidi vinatarajiwa kunufaika na mikopo ya asilimia 10 katika awamu zijazo.

Amesema taarifa ya kutengwa kwa zaidi ya Sh Mil. 400 kwa ajili ya mikopo kwa wananchi wa Mbarali ni ishara ya mafanikio ya usimamizi mzuri wa mkurugenzi huyo na jitihada zake katika kuimarisha ustawi wa wananchi.

Ndingo pia amesema mkurugenzi huyo ana mpango wa kuanzisha jukwaa maalum la vijana litakalowapa nafasi ya kuwasilisha changamoto zao pamoja na kupata taarifa za fursa mbalimbali zinazopatikana wilayani humo.

Naye mkazi wa Mbarali, Tumaini Ngota, amesema wananchi wameanza kushuhudia matokeo ya utendaji wa Mweli kupitia ziara zake katika kata na vijiji mbalimbali, ambazo zimekuwa zikisaidia kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa karibu.