Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu, ameshauri Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kujenga nyumba za bei nafuu kwa wapangaji katika jimbo la Ilala ili kuwapa wananchi makazi yanayomudu gharama na kuboresha ustawi wao.
Zungu ametoa ushauri huo wakati wa mkutano wa wananchi wa mitaa ya Kibasila na Kitonga, kata ya Upanga Mashariki, wilaya ya Ilala, ulioandaliwa na diwani wa kata hiyo, Sultan Salim, kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
“Nyumba za gharama nafuu zinawezekana na zina hadhi…….ninalishauri shirika la nyumba la taifa kujenga nyumba hizo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Ilala,” amesema Zungu.

Katika mkutano huo, wananchi waliwasilisha kero mbalimbali ikiwemo miundombinu chakavu ya maji inayosimamiwa na DAWASA pamoja na ukosefu wa alama za vivuko na pundamilia katika maeneo ya shule na maeneo mengine muhimu yanayosimamiwa na TARURA.
Zungu amesema Juni 14 atakutana na uongozi wa NHC, ukiwemo bodi ya wakurugenzi, ili kusikiliza kero za wapangaji wa shirika hilo katika jimbo la Ilala, hususan wakazi wa Upanga wanaoishi kwenye nyumba za shirika hilo.

Aidha, amesema Bunge litaendelea kuangalia uwezekano wa kuimarisha mifumo ya kisheria itakayosaidia kulinda maslahi ya wapangaji na kuhakikisha haki zao zinazingatiwa.
Kwa upande wake, diwani wa kata ya Upanga Mashariki, Sultan Salim, amempongeza Zungu kwa hatua ya kuuita uongozi wa NHC kukutana na wananchi ili kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wapangaji.

“Nashangazwa kuona baadhi ya wapangaji ambao wameishi kwenye nyumba za NHC kwa zaidi ya miaka 40 na wamekuwa wakilipa kodi kwa uaminifu wakikumbana na changamoto za kuondolewa bila kufuata taratibu za kisheria, jambo ambalo limekuwa likiwaathiri hata kiafya,” amesema Salim.
Mkutano huo pia ulijumuisha uwasilishaji wa taarifa za serikali za mitaa ya Kibasila na Kitonga pamoja na elimu kuhusu miradi ya uwekezaji ya NHC. Wadau mbalimbali walishiriki kutoa ufafanuzi wa masuala yaliyoibuliwa, akiwemo wawakilishi wa DAWASA, TARURA, NHC na mkandarasi wa huduma za usafi wa mazingira katika eneo la Upanga Mashariki.

More Stories
Kihongosi:Msibebe ajenda za Watu ambao familia zao zipo nje ya Nchi
Ndingo: Mikopo itumike kwa kazi iliyokusudiwa
Maagizo yatolewa biashara ya kaboni