July 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tututuba ahimiza matumizi ya Taasisi rasmi za fedha

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

GAVANA  wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amewahimiza wananchi kuweka fedha zao katika benki na taasisi nyingine rasmi za kifedha badala ya kuzihifadhi majumbani.

Amesisitiza kuwa amana zote zinazostahili hulindwa kupitia Bodi ya Bima ya Amana (DIB), jambo linalohakikisha usalama wa fedha za wateja hata pale taasisi ya fedha inapokumbwa na changamoto za kifedha.

Tutuba alitoa kauli hiyo mara baada ya kutembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana, ambapo alipata maelezo kuhusu majukumu ya bodi hiyo katika kulinda amana za wateja na kuimarisha imani ya wananchi kwa mfumo rasmi wa kifedha.

Ameeleza kuwa fedha zinazowekwa benki hubadilika kadri zinavyozunguka katika shughuli mbalimbali za kifedha, lakini kila mweka fedha anapaswa kuwa na uhakika kuwa fedha zake zinalindwa kwa mujibu wa sheria kupitia mfumo wa Bima ya Amana.

Amesema Bodi ya Bima ya Amana ilianzishwa mahsusi kwa lengo la kulinda amana za wateja katika taasisi za fedha, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuziamini taasisi hizo na kutumia mifumo rasmi ya kifedha kwa manufaa yao na ya uchumi wa Taifa.

Aidha, amefafanua kuwa endapo benki itafilisika au kukumbwa na changamoto nyingine za kifedha, wateja wenye amana zinazostahili hulipwa fidia kwa mujibu wa sheria, jambo linaloongeza uhakika na usalama wa fedha zao.

Tutuba pia alisisitiza kuwa Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kusimamia sera za fedha kwa weledi ili kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kuwa imara, unavutia uwekezaji na kunufaisha wananchi wote.
Mkia wa Habari

Aidha  Gavana huyo ameiasa DIB  iendelee kutoa elimu ya  kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuweka fedha katika taasisi rasmi za kifedha pamoja na nafasi ya bodi hiyo katika kulinda amana na kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha nchini.