July 10, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gavana: BoT yaendelea kumarisha uchumi Nchini

Na Joyce Kasiki

GAVANA  wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema BoT itaendelea kutekeleza sera madhubuti za fedha ili kuhakikisha uchumi wa Tanzania unaendelea kuwa imara, mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, huku ukwasi ukiendelea kuwepo kwa kiwango kinachowezesha ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam, Tutuba alisema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa wananchi kupata elimu ya kifedha, huduma mbalimbali na taarifa kuhusu mchango wa BoT katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Alisema BoT imeridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wanaotembelea banda hilo kutafuta elimu kuhusu sera za fedha, usimamizi wa sekta ya fedha, huduma za malalamiko kupitia mfumo wa Sema na BoT, pamoja na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

“Tumeona wananchi wengi wana hamu ya kuelewa namna Benki Kuu inavyosimamia uchumi, hususan kuhusu kiwango cha riba ya Benki Kuu ambacho kwa sasa ni asilimia 6.25.

Tathmini yetu inaonyesha kiwango hicho kitaendelea kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza ukwasi katika mabenki na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi,” alisema Tutuba.

Kwa mujibu wa Gavana huyo , matarajio ya BoT ni kuona thamani ya shilingi ikiendelea kuwa imara, hususan katika kipindi cha mavuno, hali itakayowasaidia wakulima kupata bei stahiki za mazao yao na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Katika ziara hiyo, Gavana huyo pia alisema BoT inaendelea kukamilisha maandalizi ya sheria na kanuni zitakazosimamia mali za kidijitali, ikiwemo sarafu za kidijitali kama Bitcoin na Stablecoins, ili kulinda watumiaji wa huduma za kifedha na kuzuia matumizi ya teknolojia hiyo katika utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

Alibainisha kuwa hatua hiyo inafanyika kwa kuzingatia uzoefu wa kimataifa na baada ya BoT kushiriki mijadala mbalimbali ya kimataifa kuhusu usimamizi wa mali hizo za kidijitali.

Aidha, alisema mfumo wa kupokea na kushughulikia malalamiko wa Sema na BoT umeendelea kupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kutoka kwa watumiaji wa huduma za kifedha, huku BoT ikiendelea kuboresha mfumo huo ili kuwafikia hata wananchi wasioweza kutumia teknolojia za kidijitali.

Tutuba alitumia fursa hiyo kuhimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kuhakikisha wanatumia mabanda mbalimbali kupata elimu ya kifedha na taarifa zinazoweza kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania, alisema taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuimarisha utulivu wa uchumi, usimamizi wa sekta ya benki, mifumo ya malipo, elimu ya fedha na upatikanaji wa huduma za kifedha nchini.

Alisema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi tulivu na mfumo imara wa kifedha unaovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.