May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RITA yavunja rekodi, yasajili vyeti vya kuzaliwa Maonesho Sabasaba

Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online,Dar

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) umevunja rekodi ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi takribani 10,495 ndani ya siku 16 katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yaliyomalizika Julai 13, mwaka huu.
Akitoa Kwa mujibu wa taarifa ya RITA iliyotolewa Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa wa RITA, Emmy Hudson safari hii wananchi wengi wameonesha mwitikio mkubwa wa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa na hii ni kutokana na kujua umuhimu hivyo wakati wa kujipatia mahitaji muhimu katika jamii yetu.

Aidha, wananchi wameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa katika maonesho hayo bila ubaguzi na usumbufu ambapo kila aliyehitaji huduma ya cheti cha kuzaliwa alipata.

Hudson ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi waliofika katika banda la RITA kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa siku ya kufungwa kwa maonesho hayo.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa RITA kuwafikia wananchi
katika kila sehemu na kutoa huduma pamoja na kwenye maadhimisho na maonesho mbalimbali kama hayo ili kuwarahisishia upatikanaji wake karibu na maeneo wanayoishi.

Hudson amesema licha ya maonesho hayo kumalizika bado wataendelea kutoa huduma hiyo katika ofisi za RITA kama kawaida, hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kufika katika ofis za RITA ili kupata vyeti vya kuzaliwa, kwani ni haki ya kila Mtanzania kuwa na cheti hicho.

Wananchi wakipata huduma katika Banda la RITA wakati wa Maonesho ya Sabasaba yaliyomalizika Julai 13, mwaka huu.

Pia, amesema RITA iko imara kutoa huduma hiyo, kwa sababu changamoto waliyoipata katika maonesho hayo ni watu kuwa wengi ambapo hata hivyo waliweza kuhakikisha kila aliyefika katika banda la RITA anapata huduma stahiki.

“Changamoto tuliyoipata ni watu kuwa wengi, ambapo ilisababisha huduma hiyo kutolewa hadi saa moja usiku, ili kila aliyefika katika banda hili aweze kupata huduma kulingana na mahitaji yake,” amesema Hudson.

Mmoja wa wananchi aliyejulikana kwa jina la Amina Abdallah ameipongeza RITA kwa huduma ambayo wameitoa na yeye kuweza kufanikiwa kupata cheti chake cha kuzaliwa kwa gharama nafuu na kwa haraka.

“Kwakweli wananchi tulikuwa wengi sana ambao tulihitaji huduma ya vyeti, lakini tulipokelewa vizuri na maofisa wa RITA waliokuwa wanatoa huduma na kutuhudumia kulingana na mahitaji yetu,naipongeza sana RITA kwa kutuletea huduma hii kwenye maonesho haya makubwa,”amesema

Naye, Joseph Mashaka amesema hakuwahi kutegemea kupata cheti cha kuzaliwa kulingana na umri wake kutokana na baadhi ya wananchi huko mtaani kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu ugumu wa kupata huduma hiyo.

“Lakini mara baada ya kufika katika banda hilo nilipewa maelekezo na kisha kuanza hatua za kupata cheti tofauti na nilivyodhani hapo awali.

“Tunashukuru kupata huduma hii hapa hapa sabasaba, Mimi ni mkazi wa Chanika kwangu ilikuwa rahisi kufika hapa kwa sababu kila nilipotamani kuifuata huduma hii katika ofisi zao nilikuwa naona uvivu kwa kuona kuwa ni mbali,” amesema Mashaka

Meya wa Jiji la Ilala, Omary Kumbilamoto alipongeza RITA kwa kutoa huduma hiyo hadi muda wa usiku kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya cheti cha kuzaliwa.

“Kazi nzuri sana mnafanya, mmejitolea kufanya kazi hadi usiku ili wananchi waweze kupata vyeti vyao kwa kufuata utaratibu, msiishie hapa tu endeleeni kupeleka huduma hii karibu na jamii,” amesema Kumbilamoto.