March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC mpya Tabora akunjua makucha, ampa kibano DED

Na Allan Vicent,TimesMajira,Online Tabora

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Bosco Ndunguru amepewa muda wa siku mbili kuhakikisha machinjio ya nyama yalioko eneo la Kariakoo yanafanyiwa usafi wa kina.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa, Dkt Batilda Buriani alipotembelea na kukagua mazingura ya machinjio hayo akiambana na Mkuu wa wilaya na viongozi wa halmashauri ya manispaa hiyo.

Amesema hali ya usafi katika machinjio hayo hairidhishi, sakafu, kuta na mifereji ya kutolea uchafu ni chafu sana na vyombo vya kuhifadhia nyama navyo haviridhishi ikiwemo uchakavu wa miundombinu.

Amesema lengo la kujengwa machinjio hayo ni kuongeza vyanzo vya mapato, lakini kwa hali ilivyo sasa malengo hayo hayawezi kufikiwa tena hivyo akaagiza maboresho makubwa yafanyike ikiwemo kuanzisha vyanzo vingine vya mapato.

RC Batilda amemtaka Mkurugenzi kutoridhika na mapato wanayopata sasa, bali wafanye kila linalowezekana ili kuhakikisha lengo la machinjio hayo kuwa kitovu cha kusafirisha nyama katika mataifa jirani ya Burundi na Rwanda linatimizwa.

“Fanyeni usafi wa kina, nawapa siku mbili tu mandhari ya machinjio haya yabadilike, pakeni rangi kuta zote, wekeni marumaru (tiles) na maboksi yote ya kuwekea nyama yawe safi, sitaki mniangushe,” amesema RC.

Amewataka kutumia sehemu ya mapato wanayokusanya kuboresha eneo hilo wakati wakisubiri mradi mkubwa wa Benki ya Dunia ambao utahusisha pia ujenzi wa machinjio hayo kwa kiwango cha kisasa.

Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Dkt Yahaya Nawanda alimhakikishia kuwa atafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha machinjio hayo yanakuwa na mwonekano mzuri ili kuongeza mapato.

Awali akitoa taarifa, Mkurugenzi Ndunguru amesema kuwa machinjio hayo yaliyojengwa kwa ufadhili wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya (European Economic Community) mwaka 1972 yanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu hali inayosababisha usafi kutoridhisha.