April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi wawatoa machozi wazazi, walezi

Na Allan Vicent,Timesmajira Online, Kaliua

UJUMBE wa kupinga vitendo vya ukatili, unyanyapaa na kutumikishwa katika kilimo cha tumbaku uliotolewa na watoto wa shule za msingi wilayani Kaliua Mkoa Tabora, umesisimua wazazi, walezi na viongozi na kusababisha watokwe na machozi.

Wakiwasilisha ujumbe huo kwa njia ya ngonjera katika kupinga vitendo hivyo kwenye mkutano uliofanyika Kijiji cha Mtakuja Kata ya Igagala wilayani hapa, imesababisha wazazi wao, walezi na viongozi mbalimbali kuguswa na ujumbe huo.

Mtoto wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Igagala namba 5, Sandra Yusuph (10) amesema dunia imejaa magonjwa mengi, watoto wanatumikishwa na wengine kubakwa bila hata aibu na kuhoji maadili ya jamii kwa watoto yako wapi.

Amesema mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, wewe unayemtesa unaharibu zawadi yako mwenyewe, mpe malezi bora mtoto wako ili akufae siku zijazo na uzeeni.

Naye mtoto Matilda Gaspar (11) wa darasa la 4 katika shule hiyo, amesema wale wote wanaowafanyia vitendo viovu watoto Mungu anawaona na hukumu itawakuta, mlezi wa watoto ni Maulana hivyo ukimtesa mtoto hutabaki salama.

Shakira Salimu (11) wa darasa la 4 katika Shule ya Msingi Igagala namba 6 amesema, utumikishwaji mtoto ni dhambi isiyo kifani iwe kwa mzazi au mlezi, anapaswa kupakatwa miguuni, kupigiwa zeze na kupewa haki yake na si kumdhalilisha.

“Mtoto ndiye taifa la kesho na mlezi wa wazazi wake, kama ataendelea kudhalilishwa, kutumikishwa au kubakwa ni nani atakayekulea wewe mzazi na taifa litaongozwa na nani?, amehoji kwenye ubeti wa ngonjera.

Oliva Norbet (10) wa darasa la 3 katika Shule ya Msingi Kakobe amesema mwanga bora kwa mtoto ni elimu, si kumpa kazi ngumu zitakazomuumiza na kumzuia kwenda shule kwani utumikishwaji watoto unaua ndoto zao.

Helena Andrea ambaye ni mkulima mkazi wa Kijiji cha Igagala namba 5 ametoa wito kwa wazazi, kubadilika na kuacha kuwatumikisha bali wawapeleke shule ili wakasome.

Mwalimu Yusuph Ramadhani wa Shule ya Msingi Igagala amesema, watoto wanapata tabu wakati wa kilimo wanawalazimisha kwenda kupalilia mashamba ya tumbaku badala ya kuwaacha wasome.

Godwin Gwasa, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igagala amewataka wazazi kutojihusisha na vitendo vya kutumikisha watoto wao katika kazi za kilimo na kuitaka serikali kutoa adhabu kali kwa wale wote ambao hawataki kubadilika.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Abel Busalama akiongozana na viongozi na wageni waalikwa wamewazawadia fedha taslimu zaidi ya sh. 50,000 na kuwapongeza kwa ujumbe mzuri, ambao umegusa kila mtu na kusababisha watokwe na machozi.

Amewahakikishia kuwa, serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mzazi au mlezi yeyote atakayebainika kumzuia mtoto wake kwenda shule.