April 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali: Hatutomvumilia atakayesababisha wananchi kukosa haki

Na James Mwanamyoto,Timesmajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amesema serikali haitomvumilia Mkuu wa Idara yeyote katika taasisi ya umma atakayesababisha mtumishi, kukosa stahili yake na mwananchi kukosa huduma bora.

Mchegerwa ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha mwaka cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, kilichofanyika Ukumbi wa Julius Nyerere Chuo cha Mipango jijini Dodoma.

Amewataka wakuu hao, kutekeleza majukumu yao kikamilifu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza viongozi katika taasisi za umma kutenda haki kwa watumishi walio chini yao na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Pia amewataka viongozi hao, kutatua kero za watumishi na wananchi pindi wanapofuata huduma katika maeneo yao ya kazi na kuongeza kuwa, pindi atakapofanya ziara kwenye maeneo yao, hategemei kukuta foleni kubwa ya wananchi wakisubiri huduma pasipokuwa na sababu ya msingi.

“Mimi, Naibu Waziri wangu na Watendaji wa Ofisi yangu tukifanya ziara katika taasisi yako, hatutegemei kukuta mlolongo wa foleni ya wanananchi wakisubiri huduma pasipo na matumaini yoyote,” amesisitiza.

Katika kutatua changamoto zinazowakabili watumishi na wananchi wanapohitaji huduma katika taasisi za umma, Mchengerwa ameanzisha mfumo wa kielektroniki unaoitwa Sema na Waziri wa Utumishi, ambao unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni ili kutoa fursa kwa watumishi na wananchi kuwasilisha malalamiko yao na kufanyiwa kazi.

“Kupitia mfumo huu, nitakuwa na uwezo wa kuona malalamiko yanayowasilishwa popote nitakapokuwa na kufanya ufuatiliaji wa namna yalivyofanyiwa kazi na ofisi yangu,” amesema.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Dugange amesema Rais Samia, amekuwa akisisitiza mara kwa mara matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi kwenye maeneo yao ya kazi.

Ameongeza kuwa ili matokeo hayo yaonekane, Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu, hawana budi kusimamia utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa umma kwa ufanisi.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kutoka kwenye Wizara, idara zinazojitegemea, wakala, taasisi za umma, Sekretariti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.