July 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga amwezesha mwenye ulemavu  Mashine kusaga viungo

Na Joyce Kasiki, Dar Es Salaam

WAZIRI  wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amemkabidhi mashine ya kisasa ya kusagia viungo mfanyabiashara mlemavu, Ester Msengi, mkazi wa Kibaha, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyompa baada ya kukutana naye katika  Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar Es Salaam.

Msaada huo unatarajiwa kuongeza tija katika uzalishaji wa viungo, kupunguza gharama za uzalishaji ,kumwondolea usumbufu wankwenda mashine na kumwezesha kupanua biashara yake.

Akizungumza Julai 13 katika banda la Wizara hiyo kwenye maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yaliyifanyika jijini Dar Es Salaam  wakati wa makabidhiano hayo, Kapinga alisema aliguswa na juhudi za Ester za kujikwamua kiuchumi licha ya changamoto ya ulemavu alionao na kuamua kuchukua hatua za haraka kumsaidia ili asiendelee kutegemea huduma za kusagia viungo kutoka kwa watu wengine.

“Tukiwa barabarani kwenye viwanja vya maonyesho ya Kimataifa ya 50 ya Biashara na kaka yangu Waziri Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara , tukamuona mama huyu akiwa na viungo kwenye kapu alilopakia kwenye baiskeli yake ya kumsaidia kutembea,tukasimama na tukamuuliza  unaenda wapi akasema anaenda kwenye banda la VETA  kwa sababu anataka mashine ya kusaigia viungo kwani wakati wa kutengeneza  viungo vyake inabidi tena atoke nyumbani aende mashine akasage arudi tena nyumbani avifanyie packaging ndio aanze kuviuza,

“Kwa hiyo sasa tukasema sisi tutamsaidia mashine ya kusagia viungo vyake na tunamshukuru sana mungu mimi pamoja na wenzangu wizarani leo tunamkabidhi mama yetu Esther mashine yake hii ya hapa ya kusagia viungo.”alisema Kapinga

Alisema serikali kupitia wizara yake itaendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo, hususan wenye mahitaji maalumu, ili waweze kukuza biashara zao na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Kapinga alisema ameridhishwa na hatua ambazo tayari zimefikiwa katika kumuinua Ester kibiashara, akieleza kuwa bidhaa zake tayari zimesajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), amepewa leseni ya biashara huku usajili wa nembo ukiendelea.

Aidha, alizielekeza taasisi zilizo chini ya wizara ikiwemo SIDO kuendelea kumpatia mafunzo ya kuongeza ubora wa bidhaa, vifungashio na kumwezesha kupata ithibati ya ubora ili bidhaa zake zipate ushindani mpana zaidi sokoni.

“Pia nawashukuru TEMDO kwa kushirikiana nasi kuhakikisha mama huyu anapata mashine hii,hatuishii hapa, nitafuatilia hadi nyumbani kwake kuona namna anavyoitumia na kuhakikisha taasisi zetu zinaendelea kumpa ushirikiano ili biashara yake izidi kukua,” alisema Kapinga.

Kwa upande wake, Ester alimshukuru Waziri Kapinga kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo, akisema msaada huo umefungua ukurasa mpya wa maisha yake ya ujasiriamali.

Alisema awali alikuwa akitumia muda na gharama kubwa kupeleka viungo kusagwa sehemu nyingine kabla ya kuvifungasha na kuviuza, hali iliyopunguza uzalishaji na faida.

“Ninamshukuru sana Waziri Kapinga kwa kuniona na kusikiliza kilio changu. Sikutegemea kama ahadi yake ingetimia kwa haraka kiasi hiki. Mashine hii itanirahisishia kazi, itanipunguzia gharama na itanipa uwezo wa kuongeza uzalishaji na kipato,” alisema Ester.

Mkurugenzi wa Huduma za Kiuhandisi Viwandani kutoka Taasisi ya Uhandisi na Usanifu wa Mitambo Tanzania (TEMDO), Elisante Mjema, alisema mashine hiyo ina uwezo wa kusaga takribani kilo 10 za viungo kwa saa, kiwango kinachoweza kuzalisha bidhaa zenye thamani ya takribani Shilingi 500,000 kwa saa.

Alisema ikiwa kutakuwa na malighafi za kutosha, Ester anaweza kufikia uzalishaji wenye thamani ya hadi Shilingi 1.5 milioni kwa siku, hatua itakayoongeza upatikanaji wa bidhaa zake sokoni na kuboresha kipato chake.