May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia arejesha mawasiliano yaliyoharibiwa na mvua Katavi

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraKatavi

KIASI cha sh. bilioni 1.1 zilizopelekwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mkoano Katavi kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja yaliyosombwa na maji ya mvua kubwa za El-nino zilizonyesha kwa wingi mkoani humo Aprili 14 na 15.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi, Martin Mwakabende, wakati akieleza jinsi walivyofanikiwa kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na el nino mkoani humo.

“Kufuatia uharibifu huo, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepeleka kiasi cha sh. bilioni 1.1 mkoani humo kwa ajili ya kazi ya matengenezo ya dharura ya miundombinu iliyoharibika,” alisema.

Amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa namna ambavyo ameuwezesha Mkoa wa Katavi kwa kupatia kiasi hicho cha fedha, ambacho kimesaidia kuhakikisha kazi ya matengenezo miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati.

“Pia tunamshukuru Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kwa namna ambavyo ameweka msukumo kuhakikisha kazi hii inakamilika, vile vile nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mha. Aisha Amour.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Katavi Aumsuri Jacob alitaja maeneo yaliyoathirika ni Barabara ya kutoka Kathuila kwenda Karema umbali wa kilomita 12 ambapo barabara iliharibika na kukata kabisa mawasiliano kila upande.

Maeneo mengine ni daraja la misunkumilo, Daraja la Stalike, Daraja la mirumba na Kilida ambapo kazi ilifanyika ndani ya siku mbili na kurejesha miundombinu yote katika hali ya kawaida.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mipango TANROADS Katavi, mhandisi Happyness Benjamin Chaji alisema kwa sasa miundombinu yote inapitika bila shida na wamejipanga kuhakikisha katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2024/2025 fedha ambayo inatolewa na Serikali inapelekwa kwenye maeneo husika ili kutekeleza mipango iliyowekwa na kuwezesha miundombinu yote kupitika wakati wote.