August 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

COPRA yazindua jarida kuongeza uelewa wa fursa kilimo

Na Joyce Kasiki,Timeamajira online,Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema taasisi hiyo imeamua kuanzisha jarida litakalotoka mara mbili kwa mwaka ili kuonesha kazi zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja na mabadiliko yanayotarajiwa katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jarida la Thamani la Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA),Mlola amesema jarida hilo litakuwa jukwaa la kuonesha thamani ya shughuli zinazofanywa na COPRA, sambamba na kuwafikia wadau mbalimbali wanaohusika katika sekta ya mazao.

Amesema uzinduzi huo ni mwanzo wa jitihada za kuendelea kusambaza taarifa kwa wadau wa ndani na nje ya taasisi ili kuongeza uelewa kuhusu udhibiti wa ubora, uzalishaji na fursa za biashara ya mazao.

Kwa upande wa wadau wa kilimo na biashara ya mazao wameeleza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa chakula, hususan uzalishaji, udhibiti wa ubora na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mshawishi wa mitandao ya kijamii
na mwanzilishi wa Mazao Connect, Fausta Mbunde, amesema wadau wanapaswa kutumia majukwaa mbalimbali kufikisha taarifa sahihi kwa vijana kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.

Mbunde amesema awali hakufahamu kuwa ubora wa zao unaohitajika kwenye masoko ya kimataifa huanzia shambani, akieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia wakulima na wafanyabiashara kuboresha uzalishaji na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya nje.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa mazao na mhamasishaji wa vijana kuhusu kilimo, biashara na uhifadhi wa mazao, Valentina Moi, amesema jitihada mbalimbali zinaendelea kuwasaidia vijana kutambua fursa zilizopo katika kilimo kwa kuwaunganisha na shughuli za vitendo kupitia ziara za mashambani.

Amesema kupitia programu za utalii wa kilimo (agrotourism), vijana wamekuwa wakipata fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu uzalishaji na biashara ya mazao, ambapo hadi sasa wamefanikiwa kufanya ziara zaidi ya 14 katika maeneo mbalimbali.