May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge ahoji utekelezwaji wa ahadi za viongozi majimboni

Na Joyce Kasiki, Dodoma 

MBUNGE wa Kwela, Deus Sangu (CCM) ameihoji serikali kwamba ni lini itatekeleza ahadi ya Viongozi wa Kitaifa ya kujenga   Barabara ya Chombe- Kaoze hadi   Kwela .

Akiuliza swali la msingi Bungeni jijini Dodoma Aprili 30 mwaka huu,Sangu amesema kumekuwa na ahadi za viongozi ya kujenga barabara hiyo lakini bado hakuna utekelezaji.

“Je ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Viongozi wa Kitaifa ya kujenga   Barabara ya Chombe- Kaoze hadi   Kwela .?” Amehoji Sangu

Akijibu swali hilo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainabu Katimba amesema Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa barabara ya Chombe hadi Kaoze  Kwela yenye urefu wa kilomita 15.

Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa  barabara hiyo inaunganisha vijiji vya Kaoze, Kiandaigonda na Chombe ambayo ipo sambamba na milima ya Lyambalyamfipa  imeathiriwa na maji ya mvua. 

“Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imekamilisha usanifu wa madaraja na barabara na kubaini gharama ya shilingi bilioni 2.3,” amesema Katimba.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kupitia fedha za tozo ya mafuta kwa ajili ya kujenga kipande cha barabara kati ya kijiji cha Kaoze na Kiandaigonda.

Naibu Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii ili kukamilisha ujenzi wa kipande cha kutoka kijiji cha Kiandaigonda hadi Chombe.

Aidha katika maswali yake ya nyongeza Sangu  alisema kuwa 

barabara ya Chombe -Kiandaigonda hadi Kaoze ni barabara ambayo imeandikiwa kuomba maombi maalumu kwa miaka miwili mfululuzo  ya shilingi bilioni 2.4 hivyo  ametaka kujua serikali ina mpango gani wa kupitia  maombi hayo  ya kuweza kupeleka fedha kwa ajili ya barabara hiyo ?

Pia amehoji mpango wa Serikali wa kuwapelekea fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.35 walizoomba katika maombi maalum kwa kutengeneza   daraja linalounganisha Kijiji cha Ilembo na Makao Makuu ya Kata ya Mpuyu .

Akijibu maswali hayo Naibu Waziri Katimba amesema Serikali inatambu uhitaji huo na maombi  ya dharura  tayari Naibu waziri ofisi ya Rais TAMISEMI aliyepita alienda  kufanya ziara katika eneo hilo pamoja na mtendaji Mkuu wa TARURA na kwamba  tayari serikali inatambua  umuhimu na ipo kwenye mchakato hivyo ombi limepokelewa na wanalifanyia kazi.