Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha Tanzania inaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani pamoja na kujenga uwezo wa taifa katika maeneo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Profesa Mkenda amesema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo amesema,Serikali imeendelea kufanya maboresho ya sera mbalimbali za sayansi na teknolojia ili ziendane na mahitaji ya sasa ya maendeleo ya dunia pamoja na kuimarisha ushindani wa taifa katika uchumi wa kidijitali.
“Serikali imefanya tathmini ya maudhui ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996, Sera ya Taifa ya Utafiti na Maendeleo ya mwaka 2010, Sera ya Taifa ya Baioteknolojia ya mwaka 2010 pamoja na Sera ya Taifa ya Teknolojia ya mwaka 2013,” amesema Profesa Mkenda.
Ameeleza kuwa tathmini hiyo imewezesha kuandaliwa kwa mapendekezo yanayosisitiza umuhimu wa kuwa na sera moja ya sayansi, teknolojia na ubunifu itakayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya taifa.
Aidha, Waziri huyo alisema Serikali imeendelea kuhamasisha ubunifu kupitia taasisi mbalimbali za elimu na utafiti nchini.
Alitaja baadhi ya bunifu zilizoendelezwa kupitia Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kuwa ni pamoja na mita ya umeme ya watumiaji wengi, mtambo wa kuzalisha haidrojeni, fimbo maalumu kwa ajili ya wasioona, mashine ya kielektroniki ya kutotolesha vifaranga pamoja na mashine ya kukata nyasi inayotumia nishati ya jua.
Bunifu nyingine ni mashine ya kufua inayotumia mfumo wa kukanyaga pamoja na mfumo wa kutengeneza mbolea ya akwaponi.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, bunifu hizo zinatarajiwa kubiasharishwa na kusaidia kuongeza ajira kwa Watanzania sambamba na kukuza uchumi wa viwanda.
Katika hatua nyingine, alisema Serikali imekamilisha maandalizi ya zana za kutathmini uwezo wa Taasisi za Umma za Utafiti na Maendeleo ili kubaini changamoto na mahitaji yaliyopo katika taasisi hizo.
Alisema hatua hiyo inalenga kuziimarisha taasisi hizo ili ziweze kuongeza mchango wake katika tafiti, ubunifu na maendeleo ya uchumi wa viwanda kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Profesa Mkenda alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu kwa kuwa maeneo hayo ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi wa kisasa na ushindani wa taifa katika dunia ya sasa ya kidijitali.

More Stories
Prof.Mbawara:TMA yakamilisha ufungaji wa mitambo miwili ya uangazi wa hali ya hewa
PBPA yapongezwa kwa usimamizi wa upatikanaji wa Mafuta nchini
Ujenzi wa Kituo cha Kupunguza Msukumo wa Mafuta Handeni wafikia asilimia 77