May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara yaomba tril 2.39 kuboresha Elimu, Teknolojia

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akiomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 2.394 kwa ajili ya utekelezaji wa mipango na vipaumbele mbalimbali vya sekta ya elimu nchini.

Akiwasilisha hotuba yake leo Mei 7,2026 Bungeni jijini Dodoma, Profesa Mkenda amesema fedha hizo zitatumika kutekeleza malengo yaliyoanishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023, inayolenga kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ujuzi kwa vijana na kuongeza maarifa ili kuendana na mahitaji ya maendeleo ya taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejipanga kutekeleza vipaumbele vitano vikuu vinavyolenga kuboresha mfumo wa elimu nchini kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu pamoja na kuimarisha maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

“Wizara itaendelea kuweka jitihada kubwa katika maandalizi ya elimu ya lazima ya miaka 10, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika elimu,” alisema Profesa Mkenda.

Ameeleza kuwa miongoni mwa maeneo yatakayopewa kipaumbele ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala mipya, kufanya mapitio ya sheria mbalimbali za elimu, kuandaa miongozo pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu na wadau wa elimu nchini.

Aidha, alisema Serikali itaendelea kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023, ambayo ilianza kutekelezwa Januari 2024 na kuzinduliwa rasmi Februari 1, 2025.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, tathmini hiyo inalenga kubaini mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sera hiyo ili kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha sekta ya elimu.

Katika hatua nyingine, Profesa Mkenda alisema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, ambapo kuanzia Januari 2028 wanafunzi wa darasa la sita na la saba watapokelewa kwa wakati mmoja katika mfumo huo mpya wa elimu.

Amesema utekelezaji wa mpango huo unafanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, hususan katika maandalizi ya miundombinu, upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na utoaji wa mafunzo kwa walimu.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo sekta binafsi katika kuhakikisha maandalizi ya utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10 yanafanikiwa kwa wakati,” amesema.

Profesa Mkenda amebainisha kuwa Serikali pia itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu sera mpya ya elimu na mitaala iliyoboreshwa ili kuongeza uelewa kwa wazazi, walimu, wanafunzi na wadau wengine wa elimu kuhusu mabadiliko yanayoendelea kufanyika katika sekta hiyo.

Amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha mfumo wa elimu nchini unazalisha wahitimu wenye ujuzi, maarifa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.