April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof Mkenda avutiwa kiwanda cha mbolea nchini Morocco

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Morroco

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda ametembele na kufanya mazungumza na uongozi wa kiwanda cha kutengeneza mbolea cha ‘Open Compute Project Foundation’ (OCP) kilichopo nchini Morocco na kuridhishwa na ubora wa bidhaa zinazotengenezwa hapo.

Akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Japhet Justine, waziri Mkenda amejionea jinsi kiwanda hicho kinavyozalisha mbolea bora kwa ustawi wa mazao.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda hicho, Prof. Mkenda mbali ya kufurahishwa na teknolojia, aliupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kufanya mapinduzi katika sekta ya mbolea na kushika namba moja kwa uzalishaji bora wa mbolea duniani kwa mwaka 2020.

“Leo nimetembelea kiwanda hiki cha OCP kujionea wanavyofanya kazi kwa ubora wa hali ya juu na kwa dhati kabisa ningependa kuwapongeza kwa hatua waliyofikia kwa kutoka kukamata namba nne kwa ubora hadi kufikia namba moja duniani mwaka 2020,” amesema Prof. Mkenda.

Kiwanda cha OCP kinamilikiwa kwa ushirikiano ambapo asilimia 50 inamilikiwa na Serikali ya Morocco na asilimia 50 zinazobaki zinamilikiwa na nchi za India, Pakistan, Ujerumani, Brazil na Ubelgiji na kutoa mchango mkubwa sana.

Katika mazungumzo yake na uongozi wa kiwanda hicho, Prof. Mkenda ameomba uongozi huo kuangalia uwezekano wa kutatua tatizo la kupanda kwa mbolea ya kukuzia mazao duniani jambo ambalo litaleta tija kwenye sekta ya kilimo.

“Moja ya jambo la msingi nililojadiliana nao ni kuona namna gani mzuri ya wao wanaweza wakatusaidia kupunguza gharama za mbolea kwa maana kwa kufanya hivyo tutakua tunamgusa moja kwa moja mkulima na kuleta tija katika sekta hii”.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa ziara hiyo imekua sehemu ya ushirikiano wa nchi mbili na sehemu ya mkakati wa Serikali katika kuboresha mazingira ya sekta ya kilimo nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji TADB, Justine ameielezea ziara hiyo kama moja ya ziara ya kujifunza na yenye kuleta matumaini chanya kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Waziri Mkenda akitembelea kiwanda cha mbolea cha OCP nchini Morocco

“Ziara hii imenipa uzoefu mkubwa kuona jinsi wenzetu walivyopiga hatua na hii kwetu imekuwa kama darasa zuri la kuhakikisha tunatengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji kwa ustawi wa sekta ya kilimo,” alisema Justine.

Waziri Mkenda na Mkurugenzi Mtendaji wa TADB wamo nchini Morocco kwenye msafara wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.