Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,
MBUNGE wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Bahati Ndingo, amevitaka vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopatiwa mikopo ya asilimia 10 kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kugombana na serikali wakati wa marejesho.
Ndingo amesema hayo Juni 6, 2026 wakati akikabidhi mikopo yenye thamani ya Sh Mil. 451.3 kwa vikundi 52 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika halmashauri ya wilaya ya Mbarali vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo hiyo.
“Ndugu zangu, mnafahamu kuwa kadri mtakavyotumia vizuri mikopo hii, ndivyo itakavyotoa fursa kwa wananchi wengine wa Mbarali ambao hawajapata mikopo hii waweze kunufaika na kufanya shughuli za uzalishaji mali,” amesema Ndingo.

Ameongeza kuwa ana imani wananchi wa Mbarali watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanaitumia vizuri mikopo hiyo ili waweze kuendelea kukopesheka siku zijazo na kutoa nafasi kwa vikundi vingine ambavyo bado havijapata mikopo hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, amesema serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza kwa vitendo utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Ni jukumu la kisheria kwa halmashauri zote 134 nchini kutoa mikopo ya asilimia 10. Hakuna mamlaka ya serikali za mitaa au mkurugenzi mwenye uwezo wa kuzuia utoaji wa mikopo hiyo, kwani mapato ya ndani yanapaswa kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wananchi,” amesema Mweli.

Amesema halmashauri itaendelea kusimamia vikundi vilivyopatiwa mikopo hiyo ili kuhakikisha vinafanikiwa kutekeleza malengo yao pamoja na kurejesha mikopo kwa wakati, hatua ambayo itawawezesha wananchi wengine kunufaika.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbarali, Brigedia Jenerali Maulidi Surumbu, amevitaka vikundi vilivyopokea mikopo hiyo kujenga nidhamu ya marejesho kwa kurejesha fedha kwa wakati kama walivyofanya wanufaika wa awali.
Kwa upande wake, Naomi Oyola, mkazi wa Chimala, amesema mikopo hiyo ina manufaa makubwa kwa wananchi kwani wengi wao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya mtaji mdogo na wengine kuingia kwenye mikopo umiza iliyosababisha kupoteza mali zao.

More Stories
Maagizo yatolewa biashara ya kaboni
Kapinga:Taka sifuri kukuza sekta ya viwanda
Londo:TBS nguzo kuu kulinda afya