June 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maagizo yatolewa biashara ya kaboni

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online- Kagera

KATIBU Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema maendeleo na ukuaji wa biashara ya kaboni hapa nchini yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesisitiza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi katika kipindi cha miongo ijayo.

Dkt. Muyungi ametoa kauli hiyo mkoani humo wakati alipokutana na wadau wa biashara ya kaboni katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wataalamu wa mazingira, wadau wa sekta binafsi pamoja na wawakilishi wa taasisi zinazojihusisha na biashara ya kaboni.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Muyungi amesema Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inasimamiwa kwa ufanisi,ili iweze kutoa manufaa ya kiuchumi kwa wananchi huku ikiendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kuanza Julai 1, 2026 unatoa nafasi kubwa kwa sekta mbalimbali, ikiwemo biashara ya kaboni, kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Amesema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususani misitu, ambayo inaweza kutumika kuzalisha mikopo ya kaboni (carbon credits),hivyo kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Amebainisha kuwa biashara ya kaboni imeendelea kuwa moja ya fursa mpya za kiuchumi duniani,kutokana na kuongezeka kwa jitihada za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa gesi joto zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali inaendelea kuweka mazingira bora yatakayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika biashara ya kaboni ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hii. Tunahitaji kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta hii unaendana na malengo ya maendeleo ya taifa na matarajio yaliyowekwa katika Dira ya 2050,”amesema Dkt. Muyungi.

Hivyo amewataka wadau wa biashara ya kaboni kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali, ili kuhakikisha shughuli zote zinazofanyika zinakuwa na uwazi, uwajibikaji na manufaa kwa pande zote zinazohusika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa KADERES, Leonard Kachebonao,amesema taasisi hiyo imeendelea kupanua ushiriki wa wananchi katika biashara ya kaboni kupitia usajili wa wakulima wadogo na utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kiuchumi.

Amesema licha ya kampuni hiyo kuwa changa, tayari imefanikiwa kusajili wakulima wadogo wapatao 180,000 katika Mkoa wa Kagera, huku zoezi la usajili likiendelea katika wilaya mbalimbali za mkoa humo,ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata nafasi ya kushiriki na kunufaika na biashara ya kaboni.

Mbali na Mkoa wa Kagera, Kachebonao amesema KADERES, imejipanga kupanua shughuli zake katika maeneo mengine hapa nchini , ikiwemo mikoa ya Morogoro na Pwani, ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika miradi ya uhifadhi wa mazingira inayozalisha mikopo ya kaboni..