Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, amesema ajenda kuu ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwafikia wananchi moja kwa moja na kujenga mahusiano mazuri kati ya viongozi na wananchi.
Mwaselela amesema hayo, wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari wa kata ya Iyela kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne, darasa la saba, kidato cha pili na kidato cha tano kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Amesema viongozi wanapaswa kushiriki kikamilifu shughuli za wananchi badala ya kujikita katika ukaguzi wa miradi pekee.

“Mahusiano yanajengwa kwa kushiriki shughuli za wananchi……….huwezi kukagua shule bila kuthamini matokeo yaliyopatikana…..wananchi walikuja kutupongeza sisi CCM kwa matokeo mazuri, lakini waliobeba mafanikio hayo ni walimu wetu na tunapaswa kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya,” amesema Mwaselela.
Amesema Rais Samia anawathamini watumishi wa sekta mbalimbali na ameendelea kuonesha dhamira ya kuimarisha sekta ya elimu, hususan kwa walimu na wanafunzi.
Mwaselela ametolea mfano utoaji wa Sh Mil. 250 kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi katika shule ya sekondari Samora, akisema uwekezaji huo unaonesha namna serikali ilivyojipanga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia Mkoa wa Mbeya.
“Si rahisi kukuta jengo kubwa na la kisasa kama hilo kila mahali,……..uwekezaji huu uliofanywa na Rais Samia katika sekta ya elimu ni ushahidi kuwa yupo karibu na wananchi, kwa hiyo kazi yetu iliyobaki ni kuwa mabalozi wa kueleza kazi kubwa inayofanywa na serikali,” amesema.
Aidha, Mwaselela amewataka madiwani wa viti maalum mkoa wa Mbeya kutembelea kata mbalimbali kueleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili watoto wa kike shuleni.

Kwa upande wake, Afisa elimu msingi wa halmashauri ya jiji la Mbeya, Andason Mwalongo, amesema kata ya Iyela imeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika sekta ya elimu kutokana na usimamizi mzuri wa walimu na viongozi wa elimu.
Amesema zaidi ya Sh Bil. 1.5 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya shule katika kata hiyo.
“Fedha hizi zinapaswa kusimamiwa vizuri ili kuhakikisha zinaleta mabadiliko chanya katika mazingira ya kujifunzia kwa watoto wetu,” amesema Mwalongo

More Stories
Dkt. Tulia ajipanga kukimbia Kilomita 42
Kikwete: Nidhamu na Uadilifu ni msingi wa maendeleo ya taifa
Madaktari Mloganzila wanufaika na mafunzo maalum ya tiba za mifupa