May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Muungano wetu ni tunu, tuulinde,tuuenzi na kuudumisha

KILA mwaka ifikapo Aprili 26, Watanzania huwa tunakumbuka siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambazo ziliungana Aprili 26, 1964, ambapo mwaka huu Muungano huu unatimiza miaka 56, huku ukiwa ni Muungano wa mfano na imara katika Bara la Afrika na ulimwenguni pote.

Waasisi wa Muungano huu ni Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ambao kutokana na umakini na maono yao waliona kuna haja ya nchi hizi kuungana huku wakizingatia usalama, utamaduni na ukaribu wa nchi hizi.

Kuna usemi wa Kiswahili usemao kuwa ‘Umoja ni nguvu na Utengano ni udhaifu’, usemi huu unasadifu Muungano wetu ambapo tunaona kuwa kutokana na kuungana kwa nchi hizi mbili na kuunganisha nguvu mafanikio mengi yamepatikana, ikiwa ni pamoja na kukuza umoja, kuzidisha maelwano na mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Uhusiano huu umejengwa kwa misingi ya ujirani wa asili, udugu na mshikamano.

Akizungumzia Muungano, hivi karibuni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),Shamsi Vuai Nahodha anasema kuwa Muungano umezinufaisha pande zote mbili,hivyo unapaswa kuheshimiwa na kuenziwa milele kwa maslahi ya kila pande.

“Nasisitiza tena, nikiwa nje ya Bunge, bila Muungano Zanzibar tungevurugana kwa kugombea ardhi.Hayati Mzee Karume tukubali aliona mbali. Uamuzi wake chini ya chama cha ASP na kuhimiza Muungano ufanyike haraka ulikuwa na maana pana”, anasema Nahodha.

Akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka 2020/2021, Waziri wa Ofisi hiyo, Musa Azzan Zungu anasema kuwa Muungano umeendelea kuleta maendeleo ya kiuchumi,kijamii na kisiasa ambayo yanayonufaisha wananchi wa pande zote mbili na kusisitiza kuwa Serikali ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuulinda Muungano na kuuimarisha ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili uzidi kuimarika.

“Serikali yetu iitaendelea kuulinda Muungano lakini tutafanyia kazi yake yote yaliyokuwa yanaonekana kama changamoto,katika utekelezaji wa masuala yanayohusu Muungano”,anasema Zungu.

Anazitaja baadhi ya changamoto ambazo zinaendelea kushughulikiwa kuwa ni pamoja na upungufu wa idadi inayostahili ya watumishi katikam kusimamia shughuli za Muungano na Mazingira,kukosekana kwa mfumo thabiti wa ushirikiano baina ya taasisi za Serikali kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu uhifadhi na usimamizi wa masuala ya mazingira na uzingatiaji mdogo wa jamii kuhusu sheria,kanuni na taratibu za uhifadhi na usimamizi wa

“Katika kukabiliana na changamoto (vikwazo) hizi,ofisi ilichukua hatua kwa kuwasiliana na ofisi ya Rais –Utumishi na Utawala Bora kwa ajili ya kuongezewa rasilimali watu,kufanya vikao vya ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais –TAMISEMI, kubaini aina ya mfumo utakaotumika kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza kazi za uhifadhi na usimamizi wa mazingira”, anabainisha Zungu.

Anaongeza kuwa Muungano ni kielelezo cha umoja katika kudumisha amani, mshikamano na usalama wa nchi ikiwa ni pamoja na kuwa nyenzo na utambulisho muhimu wa Taifa letu ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutekeleza majukumu ya msingi ya kuratibu utekelezaji wa masuala ya Muungano na kuimarisha ushirikiano katika masuala yasiyo ya Muungano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Anatoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuuthamini, kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa kwa faida za pande zote mbili za Muungano.

Watanzania hatuna budi kutembea kifua mbele na kujivunia Muungano wetu kwani ni wa mfano hasa ukilinganisha umri wake. Katika Bara la Afrika lenye nchi 54, tunaona kwamba ni nchi chache ambazo zilijaribu kuungana na muungano wan chi hizo uliparaganyika baada ya muda mfupi. Nchi kama Senegal na Gambia za Afrika Magharibi ziliungana mwanzoni mwa miaka ya 80 na kuitwa Sene-Gambia. Muungano kati ya nchi hizo mbili ulivunjika kutokana na sababu za tofauti katika uongozi.

Aidha,muungano wa nchi nyingine barani Afrika ulikuwa kati ya nchi za Ethiopia na Eritrea kuanzia mwaka 1952 hadi 1962, muungano huo ulidumu miaka kumi tu, na ulivunjika kutokana na tofauti za viongozi na ubinafsi wa viongozi wa nchi hizo. Hatima ya kuvunjika kwa muungano huo ilikuwa ni kuanza kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imedumu kwa takribani miongo miwili huku ikisababisha majanga makubwa kwa wananchi ikiwemo vifo na uharibifu wa mali.

Visiwa vya Cape Verde na nchi ya Guinua Bissau nazo zilijaribu kuungana lakini muungano huo pia ulivunjika baada ya muda mfupi sana huku sababu za kuvunjika zikiwa ni tofauti kati ya viongozi wa nchi hizo.

Kwa mifano hiyo ya nchi ambazo zilijaribu kuungana katika Bara la Afrika na kushindwa kuendeleza muungano wao,tunaona kwamba Watanzania tuna kila sababu ya kuulinda muungano wetu maana madhara ya kuuvunja ni makubwa na yenye kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wa pande zote mbili kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Hakika miaka 56 ya Muungano imekuwa na mafanikio chanya kwa Watanzania kwani mafanikio mengi yameonekana. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na fursa ya kusafiri kwa pande zote Bara na Visiwani, kuwezesha fursa za biashara na kusababisha mzunguko mkubwa wa pesa ndani ya nchi yetu kwa kupitia kubadilishana bidhaa kama vile mafuta, kahawa, matunda, vipuri vya magari na mengine mengi.

Aidha Muungano wetu,haubagui au kuwa na upendeleo wa upatikanaji wa elimu bora ambapo inatolewa bure kwa pande mbili yaani Bara na Visiwani ikiwa ni pamoja na mikopo kwa ajili ya elimu ya juu, huduma za kijamii, miundombinu ya barabara, anga na majini, huduma bora za afya, uboreshaji wa miundombinun ya afya pamoja na kujenga zahanati na vituo vya afya na ikiwemo upatikanaji wa dawa.

Mafanikio mengine ya Muungano ni pamoja na Watanzania kujenga umoja na misingi endelevu ya udugu baina yao,mifumo ya uendeshaji wa Serikali kwa uwazi chini ya demokrasia na utawala bora pamoja na kuongezeka kwa uelewa kuhusu umuhimu na faida za Muungano kwa umma wa Watanzania ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea na jitihada za kuelimisha umma kuhusu Muungano kupitia vyombo vya habari, semina, warsha,maonesho ya Kitaifa, ziara na machapisho.

Kupitia Muungano huu,miradi mbalimbali ya maendeleo imebuniwa na kutekelezwa na Serikali zote mbili. Baadhi ya mitadi hiyo ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Programu za Usimamizi wa Bahari na Pwani (MACEMP), Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Mifugo (ASDP) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA).

Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima wa nyanja za maisha yetu kwa kuwa umetufanya kuwa wamoja, kushirikiana, kushikamana na ni msingi wa amani na utulivu, maendeleo na mtangamano wetu na kwamba ndio unaotuimarisha
Ili kuhakikisha kuwa Muungano wetu hautetereki, Watanzania hatuna budi kuwaenzi waasisi wa Muungano waliotuachia urithi huu, kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwa kuwa ni nguzo na fahari pekee na ya aina yake katika Bara la Afrika.