May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA yatakiwa kulinda vyanzo vya maji

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi

MKUU wa Wilaya Nkasi Peter Lijualikali ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanavilinda vyanzo vya maji kwa kuzuia watu kulima karibu na vyanzo hivyo pamoja na kupanda miti.

Maagizo hayo ameyatoa leo alipokuwa akitembelea na kukagua miradi ya maji ambapo ameweza kutembelea mradi wa maji Kabwe, Matala,Kirando na Mkinga.

Ambapo amesema kuwa vyanzo vyote vya maji inabidi vilindwe ipasavyo na kuhakikisha shughuli mbalimbali za kibindamu zinafanywa mbali na vyanzo hivyo.

Amesema kuwa ili miradi hiyo iweze kudumu na kuleta tija kwa jamii ni lazima itunzwe kisheria na wananchi waweze kupata maji wakati wote kama ilivyo ndoto ya Rais Samia ya kumtua ndoo Mama kichwani .

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, Kaimu Meneja wa RUWASA wilayani Nkasi Jaffari Amri amesema kuwa miradi mitatu ya maji ya Kabwe,Kirando na Mkinga imepata changamoto baada ya maji ya ziwa Tanganyika kuvamia vyanzo vyake vya maji.

Amri amesema kuwa mradi wa maji Kabwe umepata changamoto baada ya maji ya ziwa Tanganyika kuvamia vyanzo vya maji na kupelekea mfumo wa kuendesha mitambo kuwa ndani ya maji na kushindwa kufanya kazi.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya baada ya kupokea taarifa hiyo amemtaka Katibu Tawala wa Wilaya hiyo kuhakikisha anamuandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji kumweleza uhalisia wa hari ya miradi hiyo ili kuona namna ya kupata fedha ili waweze kuihamisha mifumo ya mitambo kutoka kwenye maji ili iendelee kufanya kazi.

Amedai kuwa miradi hiyo kusimama kufanya kazi kunawatesa wananchi na ipo haja kwa serikali kulifanyia haraka jambo hilo ili maji yaendelee kutoka na kuwaondoa Wananchi kwenye janga la maradhi ya milipuko kwa kuendelea kutumia maji yasiyo salama.