May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRB kuanza oparesheni ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na wakandarasi wa kigeni

Na.Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imesema inaanza operesheni maalum ya kukagua miradi mikubwa inayotekelezwa na Makandarasi kutoka nje ya nchi, kutokana na miradi mingi kutekelezwa chini ya viwango.

Aidha imebaini hayo kufuatia ziara mbalimbali za Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa katika miradi mbalimbali ikiwemo barabara ambayo imeonekana thamani yake kuwa ndogo.

Akizungumza leo jijini Arusha, katika mafunzo ya usiamizi wa fedha kwa Makandarasi,Msajili wa CRB, Rhoben Nkori, amesema bodi hiyo imeamua kufanya operesheni hiyo maalum kuanzia Mei hadi katikati ya Juni mwaka huu.

Hivyo operesheni hiyo maalum ni kwa ajili ya kujiridhisha wakandarasi wote walioingia mkataba na serikali kama wanafanya kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na sheria,kinyume na hapo hatua zitachukuliwa.

“Bodi iemamua kufanya operesheni maalum ya kutembelea miradi na kukagua miradi yote mikubwa inayofanywa na wakandarasi wa nje ambayo mingi hufanywa nao,tumefuatilia ziara za Waziri wa ujenzi amepita katika miradi mingi ya barabara ambayo tunaona inatekelezwa tofauti na ambavyo bodi inategemea kwani tulitegemea wakandarasi ni wakubwa na wanafanya miradi kama walivyoingia mikataba na kwa muda unaotakiwa,” ameeleza na kuongeza kuwa


“Baada ya kufuatilia ziara ya Waziri tumeamua kama Bodi kupitia miradi hii na kujifunza utekelezaji thabiti kwa wakandarasi waliofanya vizuri ili kujifunza mbinu walizotumia zisaidie kwa wakandarasi wazawa pia kuangalia makandarasi hawa ambao wanafanya kazi kwa kusuasua na tumewasajili kwanini wanafanya miradi chini ya kiwango au kufanya kinyume na tutakagua tukijiridhiishisha kazi wanazofanya haziendani na mikataba waliyoingia na kama sheria yetu itaturuhusu kuchukua hatua kwa kuwaondoa kwenye usajili kama ambavyo tuliwaingiza,”.

Meneja wa CRB Kanda ya Kaskazini, Sauda Njila amesema mafunzo hayo ya siku tatu yatakutanisha wadau 150 ambapo yatasaidia sekta hiyo ya ujenzi hapa nchini hasa Makandarasi wazawa.

Amesema mafunzo hayo hutolewa kufuatia tafiti mbalimbali ambapo wamebaini Makandarasi wakipata mafunzo mbalimbali yatawasaidia
kuboresha utendaji kazi wao na kuwa na matokeo mazuri.

“Matarajio ni kwamba wakitoka hapa watakuwa wamebobea kwenye masuala ya usimamizi wa fedha kwani ni muhimu ili kuendelea popote lazima uweze kusimamia fedha na biashara yoyote inahitaji mafunzo ya usimamzii wa fedha kwa sehemu yao wanahitaji mafunzo haya ili wajue mgawanyiko wa fedha zao na kutekeleza miradi kwa wakati na isisababishe miradi kutokamilika kwa wakati,”.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makandarasi na watoa huduma ShirikishiTanzania (TUCASA), Mhandisi Yahaya Mnali, amesema mafunzo hayo ni muhimu na yana manufaa kwani yatasaidia kuboresha fani hiyo na
kutekeleza wajibu wao kikamilifu.

“Kabla ya mafunzo haya inawezekana kazi zilikuwa zinafanyika,matokeo yake zinaonekana dosari za hapa na pale labda zilitokana na kutofahamu
masuala mengine ikiwemo usimamizi wa fedha,tukifanya kazi kwa ubora tutaaminiwa na tutakuwa na uwezo wa kufanya kazi kubwa na tutakuza uchumi wetu,”.