May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utafiti wa mafuta Bonde la Eyasi Wembere

Gesi asilia ni nafuu, rafiki kwa mazingira

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio

Na Godfrey Ismaely

GESI asilia ni mchanganyiko wa molekuli nyepesi nyepesi za Carbon na Hydrogen mfano methane (CH4) na Ethane (C2H6). Aidha, gesi asilia inatokana na kuoza kwa mata ogania (organic matter) kama vile uozo wa masalia ya mimea na wanyama walioishi miaka mingi iliyopita.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache Duniani yaliyobarikiwa kuwa na gesi asilia kwa wingi ambapo kufikia sasa kiasi cha gesi asilia futi za ujazo trilioni 57.54 zimegundulika nchini.

Jukumu la kuisimamia gesi hiyo na kuisambaza kwa watumiaji mbalimbali wakiwemo wa majumbani, magari, taasisi pamoja na viwandani kwa ajili ya matumizi hapa nchini linasimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio anasema, gesi asilia inapatikana katika ardhi kwenye mwamba wenye vinyweleo vingi ulioko chini ya ganda la mwamba imara zaidi unaozuia gesi kupanda juu zaidi.

Dkt.Mataragio anasema, sifa hiyo huipa upekee gesi asilia na kuitofautisha na gesi zingine ambazo zinatumika hapa nchini kama vile gesi za mitungi ambazo hupatikana baada ya usafishaji wa mafuta ghafi kwa mataifa yaliyogundua mafuta.

Anabainisha kuwa, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ni Shirika la Umma lililoanzishwa mwaka 1969 kwa Agizo la Rais Na. 140 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma ambalo limekuwa likifanya juhudi mbalimbali kuhakikisha gesi asilia inayogundulika inawafikia na kuwanufaisha Watanzania.

“Shirika lilianzishwa pamoja na mambo mengine kwa ajili ya kulinda maslahi ya Taifa katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.

“Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania linajishughulisha na utafutaji, uchimbaji, uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mafuta na gesi na usambazaji kwa wateja,”anafafanua Mkurugenzi Mtendaji huyo.

Dkt.Mataragio akifafanua zaidi kuhusu gesi asilia anasema, gesi hiyo inasifika kwa ubora hasa katika uhifadhi wa mazingira ikilinganishwa na aina nyingine ya nishati kama vile mkaa,kuni pamoja na mafuta mazito.

Kituo cha kujazia gesi ya magari

ìGesi hiyo husambazwa kwa ajili ya matumizi ya majumbani, magari na viwandani kwa kutumia mabomba maalumu, ambayo hutandazwa hadi kumfikia mteja.

“Baada ya kumfikia mteja, kifaa maalumu (mita) hufungwa ili kubaini kiasi cha gesi ambacho mteja amekitumia, utaratibu ambao huwa katika mfumo wa lipia huduma kwanza yaani kwa wateja wa majumbani ambapo mteja anaweza kununua kiasi cha gesi cha kuanzia sh.1,000,îanasema Dkt.Mataragio.

CHANGAMOTO USAMBAZAJI

Dkt.Mtaragio anasema mbali na mafanikio waliyoyapata mpaka sasa bado zipo changamoto ikiwemo ufinyu wa bajeti itakayowawezesha kusambaza gesi,wataalamu wa utengenezaji miundombinu na uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya gesi.

ìUsambazaji sasa tunafanya na kampuni tanzu ya TPDC, GASCO hali inayosababisha kasi kuwa ndogo. Hivyo kwa kulitambua hilo, kwa sasa tupo kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali binafsi ikiwemo kampuni ya Japan ambao ni wataalamu wa gesi kwa muda mrefu,îanasema.

KIWANGO CHA GESI

Kisima cha gesi

Kulingana na takwimu za makadirio za mwaka 2008 gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 175,400,000 ziligundulika katika maeneo mbalimbali duniani, Urusi ikiwa kinara kwa kuwa na akiba ya gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni 44,650,000.

Anasema, kwa Tanzania, utafiti wa mafuta na gesi ulianza miaka ya 1950 ambapo tafiti mbalimbali zilifanyika kupitia makampuni ya kigeni.

Kufikia mwaka 1974 gesi asilia ya kwanza nchini Tanzania iligundulika katika kisiwa cha Songosongo kilichopo katika Bahari ya Hindi Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi,kufikia sasa kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia zimegundulika nchini.

FEDHA ZAOKOLEWA

Dkt.Mataragio anasema, kwa kiasi kikubwa asilimia 80 ya gesi asilia inayozalishwa nchini inatumika katika kuzalisha umeme ambapo katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 kiasi cha umeme kilichokuwa kinazalishwa kwa kutumia gesi asilia kilikuwa ni chini ya megawatt 400 na kufikia mwaka 2020 zaidi ya megawatt 892 sawa na asilimia 97 katika gridi ya taifa kinazalishwa kwa kutumia gesi asilia.

ìTangu kuanza kutumika kwa gesi asilia kwa matumizi ya uzalishaji wa umeme nchini, TPDC imewezesha kuokolewa kwa fedha kiasi cha sh.trilioni 30.22,îanasema.

Fedha hizi ziliokolewa baada ya gesi asilia kuanza kutumika katika uzalishaji wa umeme nchini badala ya mafuta mazito yaliyokuwa yanaagizwa nje ya nchi kwa lengo la kuzalisha umeme nchini.

Dkt.Mataragio anasema, uchakataji wa gesi asilia kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya uzalishaji wa umeme nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kuondokana na mgawo wa umeme na hivyo kusaidia kutekeleza dhana ya Tanzania ya viwanda kwa vitendo kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika.

WANUFAIKA

Meneja Rasilimali Watu wa Kiwanda cha Lodhia kilichopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Martin Mnkande anasema, matumizi ya gesi asilia katika kiwanda hicho yamesaidia kwa kiwango kikubwa katika uhifadhi wa mazingira na kupunguza gharama za uzalishaji kwa upande wa nishati.

“Kabla ya kuanza kutumia gesi ya TPDC tulikuwa tunatumia mafuta mazito kwa ajili ya nishati na ilikuwa inatoa moshi mwingi ambao ulikuwa unachafua mazingira kwa kiwango kikubwa.Lakini baada ya kupata gesi asilia, mabo yamebadilika kwa kiwango kikubwa kuanzia uzalishaji hadi uhifadhi wa mazingira,”anasema.

Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Arun Lodhia anasema, kwa sasa matumizi ya gesi asilia katika kiwanda hicho yameokoa gharama za uendeshaji kwa asilimia 30 ambapo kabla ya matumizi ya gesi kiwanda hicho kilikuwa kikitumia kiasi cha lita 50,000 hadi 60,000 za mafuta mazito kuzalisha nishati.

ìTunafanya mpango ili kuagiza mitambo inayotumia mifumo ya gesi asilia katika utendaji. Ukiangalia kwa sasa tunailipa TPDC sh.milioni 160 kwa mwezi kwa ajili ya gesi, lakini Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tunalipa sh.bilioni 1.255, hivyo kwetu matumizi ya gesi yatatuletea faida kwa kupunguza gharama zaidi,îanasema.

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu anasema, Serikali kupitia TPDC ina mpango wa kuongeza kasi ya kuviunganishia gesi viwanda vingi zaidi kwa siku chache zijazo.

“Tumeanza na viwanda vya Mkuranga ambavyo mradi wa bomba la gesi limepita na tutaendela katika mikoa mingine zaidi kufanikisha matumizi ya nishati hii,”anasema.

Katika ziara ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ya kutembelea maeneo yanayonufaika na gesi asilia jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula anasema, lazima TPDC iongeze juhudi katika usambazaji wa gesi kwa wananchi.

ìTunawapongeza kwa juhudi zinazoonekana za kuwezesha gesi hii asilia kufika kwa wananchi na kuanza kutumika bila tatizo lolote,wananchi wameonesha kufurahishwa na juhudi za uunganishaji wa nishati hii.

“Lazima muongeze juhudi,mna malengo ya kuwafikia watu 10,000 kufikia 2021 mpaka sasa mmefikia watu 1,385 juhudi zinahitajika ili kufikia malengo haya,îanasema.