Na Joyce Kasiki, Dodoma
SERIKALI imeanza utekelezaji wa Mradi wa sekta ya uvuvi wa BahariĀ (TASFAM) wenye thamani ya dola za Marekani milioni 117 zilizotolewa kwa mkopo na Benki ya Dunia, ukiwa na lengo la kuboresha mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya uvuvi wa bahari nchini kwa kipindi cha miaka mitano.
Akizungimza na waandishi wa habari katika maonyesho ya Wakukima na Wafugaji Nanenane Nzuguni jijini Dodoma,Mratibu wa Mradi wa TASFAM, Dkt Nicholas Mlalila, amesema mradi huo unatekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar na unalenga kuimarisha uzalishaji, uchakataji, masoko na miundombinu ya uvuvi ili kuongeza tija na kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.
Amesema sehemu kubwa ya fedha hizo zitaelekezwa katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya uvuvi ikiwemo mialo ya kisasa, hatua itakayosaidia kupunguza upotevu wa samaki unaotokea katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi.
Dkt.Mlalila amesema mradi huo pia utatoa mikopo kwa wadau wote wa mnyororo wa thamani wa uvuvi kupitia Benki ya Biashara Tanzania (TCB), ambapo wavuvi na wafanyabiashara watawezeshwa kupata boti, pembejeo, vifaa vya kuhifadhia samaki kwa baridi pamoja na mitaji ya biashara.
Aidha, amesema mradi utajenga kituo kikubwa cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika eneo la Kunduchi, kitakachozalisha aina mbalimbali za vifaranga pamoja na kuendeleza kilimo cha mwani na kufanya majaribio ya ufugaji wa viumbe vya majini kwa kutumia vizimba.
Kwa mujibu wa Dkt.Mlalila, TASFAM pia utaimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi kwa kuunda vikundi vya usimamizi wa maeneo ya uvuvi, kuviwezesha vyama vya ushirika na kushirikiana na taasisi za kifedha ili kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo.
Ameongeza kuwa mradi utaimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu za uvuvi kwa kushirikiana na maafisa uvuvi katika wilaya zote za ukanda wa pwani, hatua inayolenga kuongeza ubora wa taarifa za uzalishaji na mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.
Dkt.Mlalila amesema Serikali ina matarajio kuwa baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo kutakuwa na ongezeko la uzalishaji, kupungua kwa upotevu wa mazao ya uvuvi, kuimarika kwa kipato cha wavuvi pamoja na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

More Stories
Dkt.Nungu:Haki za wabunifu zilindwe
EWURA yasihi matumizi salama ya umeme na LPG
T-CAMS yaleta mapinduzi sekta ya uwakala wa forodha