August 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Amana za Benki zinalindwa hadi Milioni 7.5

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

BODI  ya Bima ya Amana (DIB) imesema amana za wateja katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinalindwa kwa kiwango cha hadi shilingi milioni 7.5 endapo benki itafilisika au kufutiwa leseni.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima na wafugaji  Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma,.

“Kiwango hicho kinahakikisha mteja mwenye amana zisizozidi shilingi milioni 7.5 analipwa fedha zake zote ikiwa benki yake itafungwa.”amesema Mwambande

Amesema Mfuko wa Bima ya Amana huchangiwa na benki pamoja na taasisi za fedha zinazopokea Amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila benki huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake mara moja kwa mwaka.

Mwambande amesema fedha zinazokusanywa huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wateja pale benki inaposhindwa kuendelea na shughuli zake.

Aidha, amesema kwa sasa DIB inaendesha ufilisi wa benki tisa zilizofungwa kati ya mwaka 2000 na 2018 ambazo ni Greenland Bank, Delphis Bank, FBME Bank, Efatha Bank, Covenant Bank for Women, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank na Kagera Farmers Cooperative Bank.