April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

“Michezo ni afya,ajira” -DC.Ngubiagai

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online -Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai,amesisitiza watoto na vijana walio ndani na nje ya shule kushiriki michezo kwani ni chanzo cha afya bora, na ajira.

Pia wakati mwingine hutumika kutangaza maeneo ambapo michezo ya aina flani hufanyika.

Cde.Ngubiagai,ameyasema hayo wakati akipokea mipira 146 kutoka shirika lisilo la kiserikali la Sports Charity Mwanza, linalojihusisha na masuala mbalimbali ya michezo na kuikabidhi kwa walimu wa michezo wa vituo vya michezo vilivyotengwa kwa ajili maandalizi ya michezo ya UMITASHUMITA na UMISETA.

Cde.Ngubiagai amepogeza shirika hilo kuunga mkono juhudi za ukuzaji wa sekta ya michezo ndani ya Wilaya ya Ukerewe huku akimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuifanya michezo kuwa kipaumbele katika shule zote za msingi na sekondari .

“Taifa ambalo halina wanamichezo litashindwa kujitangaza ,litashindwa hata kujitengenezea utamaduni wake lenyewe,”amesema Cde.Ngubiagai.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Singisbert Themistocles,amewataka walimu waliokabidhiwa mipira hiyo kuitunza vizuri na kuitumia ipasavyo.

Mkuu wa shule ya sekondari Busangumugu iliyopo Kata ya Ilangala,Mwl.Peter Eliya,amesema michezo inasaidia kuchangamsha akili za watoto sambamba na kukuza vipaji,hivyo kupunguza utoro shuleni kwa baadhi ya maeneo.